Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliyopo katika Hoteli ya Edema, Mkoani Morogoro, Disemba 29, 2020.
Sehemu ya Wajumbe wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) wakifuatailia kwa amakini hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) walipokuwa kwenye Mkutano Mkuu wa Sita (6) wa Taifa.
Baadhi ya Wageni waalikwa wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Bw. Paul Sangeze (kulia aliyesimama) akieleza kuhusu madhumuni ya mkutano huo mkuu wa TUICO uliofanyika Mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea hotuba ya risala mara baada ya kusomwa na Mkuu wa Idara ya Sheria (TUICO), Ndg. Noel Nchimbi alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Pendo Berege akieleza jambo wakati wa mkutano huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wengine TUICO na Serikali pamoja na wadau mbalimbali baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika Mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia) akizungumza na baadhi ya wajumbe walioshiriki mkutano huo. Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Ndg. Tumaini Nyamuhokya.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
*************************************************
Na: Mwandishi Wetu, Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka waajiri nchini kutoogopa uwepo wa Vyama vya Wafanyakazi katika sehemu za kazi kwa kuwa ndio fursa ya pekee ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika sehemu za kazi.
Ametoa kauli hiyo hii leo Disemba 29, 2020 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliyopo katika Hoteli ya Edema, Mkoani Morogoro.
Waziri Mhagama alieleza kuwa Vyama vya wafanyakazi vimekuwa tegemeo kwa wafanyakazi hususan katika kulinda na kutetea maslahi na haki za wafanyakazi waliopo nchini, hivyo wajibu wa waajiri kutambua uwepo wa vyama vya wafanyakazi ili kuleta tija katika sehemu za kazi.
“Uwepo wa Vyama Vya Wafanyakazi imekuwa ni nyenzo muhimu ambayo imeongeza tija na kujenga hali ya msukumo katika utendaji wa kazi wa wafanyakazi waliopo katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini,” alieleza Mhagama
Alifafanua kuwa, vyama vya wafanyakazi ni umoja wa hiari na wa kidemokrasia ambao wafanyakazi wamekuwa wakitumia kulinda na kupeleka mbele mahitaji na matakwa ya pamoja kwa waajiri wao.
“Tumeshuhudia namna baadhi ya vyama vya wafanyakazi vimekuwa chachu katika kuhamasisha majadiliano baina ya waajiri na wafanyakazi katika kufunga mikataba ya hali bora ya kazi ambayo imekuwa ikiwanufaisha wanachama,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa, vyama vya wafanyakazi vijenge utaratibu wa kuandaa mpango kazi wa muda mrefu na wa muda mfupi ili kutimiza malengo ya vyama hivyo vinavyowawakilisha wafanyakazi kwa wakati. Pia amehimiza suala la utoaji wa elimu kwa wanachama wa vyama vya wafanyakazi ili kuwapa wanachama wao uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vyao.
“Mkiwaelimisha wanachama mtajenga uthubutu wa kusimamia masuala mbalimbali na mtawajengea ujasiri wanachama wenu kwa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi,” alisema
Sambamba na hayo amevitaka vyama vya wafanyakazi kusimamia misingi ya sheria, maudhui ya uwepo wa taasisi zao na sekta zao badala ya kuanzisha migogoro isiyokuwa na sababu ambayo itapelekea waajiri kuogopa uwepo wa vyama vinavyowawakilisha katika maeneo ya kazi.
“Matumaini yangu vyama vya wafanyakazi vitajenga mahusiano mazuri baina ya wafanyakazi na waajiri ili kupunguza migogoro iliyopo katika sehemu za kazi,” alisema Mhagama
Pia, Waziri Mhagama amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi vilivyopo nchini kujenga utaratibu wa kukumbushana wajibu wao kama viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao sawasawa katika maeneo wanayoyawakilisha.
Aidha, pongezi nyingi zilitolewa kwa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) na Mheshimiwa Mhagama ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kutokana na namna chama hicho kimekuwa kikiratibu shughuli zake, pamoja na kuwatakia uchaguzi wenye amani na utulivu ambao ulifuata baada ya ufunguzi wa mkutano huo.
Kwa Upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Ndg. Tumaini Nyamuhokya alieleza Serikali imekuwa msatri wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini akitolea mfano suala la punguzo la kodi “Pay as You Earn” ambalo limewanufaisha wafanyakazi waliopo katika sekta binafsi na sekta ya umma.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Bw. Paul Sangeze alifafanua kuwa TUICO ni miongoni mwa Vyama huru kumi na moja vya wafanyakazi nchini ambavyo vitaendelea kuboresha hali ya wanachama na wafanyakazi wakati wote wakiwa makazini.
“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na serikali pale tutakapoona kuna haja ya kutunga sheria sahihi za kazi na kuandaa sera nzuri za kuendeleza uchumi na manufaa kwa wafanyakazi,” alieleza Sangeze
Pia, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Karubelo alieleza kuwa tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani kumekuwa na mshikamo mkubwa na amani miongoni mwa waajiri na wafanyakazi ambayo imepelekea wafanyakazi kupata heshima kubwa na tunashuhudia wafanyakazi wakishiriki kwenye miradi mkubwa ambayo inatekelezwa hapa nchini.
Naye, Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Pendo Berege alisema kuwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa katiba na ndio sehemu pekee ya kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu chama.
“Ofisi ya Msajili inategemea kuona vyama vya wafanyakazi nchini vinaendelea kutekeleza katiba za vyama vyao, kutambua mipaka ya kiutendaji na kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama,” alisema Berege
Mkutano huo Mkuu wa wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika Mkoani Morogoro ilikuwa ni sehemu mmoja wapo ya utekelezaji wa mikutano kwa mujibu wa katiba ya Chama ambapo tukio hilo lilihusisha na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.