“TATIZO LA MAJI LINAKWENDA KUISHA KABISA”- MHANDISI SANGA

 

*******************************************

Na. Beatrice Sanga- MAELEZO

Katibu Mkuu Wizara ya Maji  Mhandisi Antony Sanga  ameeleza kuwa tatizo la upatikanaji wa maji kwa wananchi linakwenda kuisha kabisa kwa sababu miradi mingi ya maji iliyokuwa inajengwa katika awamu hii ya tano imekamilika na mingine imefikia hatua za mwishoni hali itakayopelekea upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini.

Mhandisi Sanga ameyasema hayo hii leo alipokuwa akifungua mkutano wa nne wa Kitaifa wa sekta nyingi juu ya usimamizi wa vyanzo vya maji (4th national mult sectoral forum on water sources management) uliowakutanisha wadau mbalimbali wa maji. Mkutano huo una lengo la kuongeza na kujenga ushirikiano kati ya wahusika na kuangazia pande zinazoweza kutumika katika usimamizi wa rasilimali za maji.

Ameongeza kuwa mijadala mbalimbali inayokutanisha wadau wa maji inasaidia namna bora ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi ambao hawapati huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika ambapo Serikali inaenda kutengeneza mabwawa na mito mikubwa katika maeneo kame na kumaliza tatizo la maji katika maeneo hayo.

“Tunachokwenda kufanya sasa hivi kwa kutumia mijadala hii mbalimbali tunakwenda kupata kitu kizuri cha namna bora zaidi ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi ambao hawapati, yale maeneo kame tunakwenda kujenga mabwawa lakini tunakwenda kutengeneza mito mikubwa katika maeneo ambayo yana vyanzo vinavyoonekana ili kuhakikisha wananchi wengi ambao hawana maji wanapata kwa uhakika”, amesema Mhandisi Sanga

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa linalowakutanisha wadau wa maji, Mhandisi Mbogo Mfutakamba ameeleza kuwa nchi inaendelea kupiga hatua kwa kuhakikisha inakuwa na maji endelevu ambapo mpaka sasa wastani wa upatikanaji wa maji safi na salama umepanda na kufikia asilimia 70.1 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 86 kwa maeneo ya mijini.

“Kwa sasa maeneo ya  vijijini tuna wastani ambao unafikia asilimia 70.1 ya matumizi bora ya maji safi na salama, lakini kwenye maeneo ya mijini tumepanda kidogo na kufikia asilimia 86 na kwa viwango ambavyo tumejiwekea tutafika asilimia 95”, amesema  Mhandisi Futakamba

Naye Balozi wa Canada nchini Tanzania Bi. Pamela O’Donnell ameshukuru kupata nafasi ya kufanya kazi na Tanzania katika masuala ya kimaendeleo ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa na kujadili namna ya kupata suluhisho kupitia majukwaa mbalimbali.

Kongamano la Sekta nyingi la 2020 linakuja wakati ambapo maendeleo mazuri yametekelezwa katika usimamizi wa rasilimali za maji licha ya kuongezeka kwa hitaji la sekta na ushiriki mwingine wa wadau. Septemba 2020 Tanzania ilishiriki katika zoezi la ulimwengu lililoongozwa na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP)  juu ya kiwango cha utekelezaji wa usimamizi jumuishi wa rasilimali za maji (SDG6.5.1) ambapo Tanzania ilipata wastani wa alama 54 kati ya kiwango cha juu cha 100 na hivyo kugawanywa chini ya jamii ya kiwango cha kati.

Post a Comment

Previous Post Next Post