DARAJA LA BUSISI SASA DARAJA LA J.P.MAGUFULI BRIDGE

 

****************************************

NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza

Daraja la Kigongo-Busisi linalojengwa kwa kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita katika Ziwa Victoria limepewa jina la J.P.Magufuli Bridge.

Daraja hilo linajengwa ndani ya ziwa likiunganisha Barabara ya Usagara – Sengerema – Geita ambazo ziko kwenye Ushoroba wa Ziwa Victoria kuanzia Sirari mpakani mwa Kenya hadi Mutukula mpakani mwa Uganda,  umbali wa km 774.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale ametangaza jana jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa Mkuu wa Mwanza John Mongela.

Alisema daraja hilo linalojengwa ndani ya Ziwa Victoria kwa gharama ya sh. bilioni 699.2 likiunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza,litaitwa Daraja la J.P.Magufuli (J.P Magufuli Bridge).

Mhandisi Mfugale alisema Rais Magufuli ana historia kubwa na daraja hilo ambalo limeghrimu maisha ya wananchi waliokuwa wakivuka kwenda ng’ambo ya pili wakitumia mtumbwi kutokana na vivuko kuhribika lililompa shida, hivyo  kuliita kwa jina litafahamika zaidi duniani.

Alisema kuwa wameona daraja hilo liitwe kwa jina la J.P. Magufuli ingawa yeye hajarauhusu na pia kwenye mikataba ya ujenzi wa mradi huo wa kisasa imeandikwa hivyo,hawezi kustaafu hadi daraja hilo likamilike maana Rais Magufuli analifuatilia sana kwa sababu watu walifariki baada ya kupanda mtumbwi wakivuka kwenda ng’ambo ya pili,jambo  ambalo lilimpa shida sana.

Mtendaji Mkuu huyo wa TANROADS alisema daraja hilo litakamilika Februari 24, 2024, utekelezaji wake umefikia asilimia 11.18 kulinganisha na asilimia 17.14 zilizopangwa kufanyika huku vifaa vyote vinavyohitajika vikiwa vimefikishwa kwenye eneo la mradi.

Kwa upande wake Mongela alisema historia ya daraja hilo ni ndefu nchini na linatajwa mno baada ya kupoteza maisha ya watu,hivyo Rais aliamua kulivalia njuga kuhakikisha linajengwa na kukamilika, licha ya kuwepo vivuko na nguvu kubwa ya serikali litasaidia uchumi wa mkoa na kuchangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi kwa kuwa litamgusa kila mwananchi katika kuongeza uchumi na maendeleo ya Mkoa wa Mwanza.

Mongela alieleza kuwa Rais Magufuli ana mapenzi na huruma kwa wananchi wake ambapo daraja hilo ni la kiuchumi na kwenye uchumi gharama nyingi za bidhaa na huduma kwa kiwango kikubwa ni usafirishaji, hivyo daraja hilo kuitwa jina la J.P.Magufuli Bridge litaweka heshima stahili ya juhudi zake za uwekezaji wa sh. bilioni 716.533.

Alisema historia hiyo itaishi milele na itakuwa kumbukumbu kwa vizazi vya sasa na vijavyo vitapata kipimo cha uzalendo na kujitoa kuwa aliwahi kuwepo mzalendo katika nchi hii aliyejenga miradi ya Bwawa la umeme la Nyerere, SGR,maji na elimu.

Aidha  Rajabu Ngazi,alisema daraja hilo litawasaidia kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa sababu fursa nyingi zitapatikana.

Alidai vivuko vilipokuwa vinaharibika vilikwamisha mambo mengi ya maendeleo na kiuchumi, mazao yaliharibika kwa kukaa saa 8 hadi 10 kusubiri kivuko,sasa watafanya biashara,utalii wa ndani na nje kwenye daraja hili, uchumi wa watu utaimarika na hakuna mtu atshindwa kutembele daraja hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post