Wizara ya Kilimo imefanikiwa kupata soko la mahindi ya njano takribani tani milioni moja kwa mwaka nchini Misri kuanzia mwezi Julai mwaka 2021 kupitia kampuni ya Smart Group ya Misri.
Taarifa hiyo imetolewa jana (16.11.2021) jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia kikao alichofanya na Mwenyekiti wa kampuni ya Smart Group ya nchini Misri Yasser Attia aliyetembelea Tanzania kutafuta masoko ya mazao ya nafaka.
Kusaya alisema Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Misri umeweza kufanikiwa kuwashawishi wafanyabiashara hao kuja Tanzania kuona na kujadili fursa za masoko ya wakulima ili kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao.
“Kampuni ya Smart Group toka Misri imekubali kununua mahindi ya njano tani milioni moja toka kwa wakulima wa Tanzania kuanzia mwezi Julai 2021 kufuatia mazungumzo yetu leo hapa Dodoma “alisema Kusaya
Katibu Mkuu Kusaya aliongeza kusema mahindi ya njano yanayotakiwa na kampuni hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha chakula cha mifugo na samaki hali inayotoa fursa kubwa kwa soko la Tanzania kwa kuwa watanzania wengi hawali mahindi ya njano
Kusaya alisema kwa sasa uzalishaji wa mahindi ya njano nchini ni mdogo hatua ambayo itakuwa ni fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mahindi haya.
“Uhalisia uliopo sasa ni kuwa uzalishaji wa mahindi ya njano ni mdogo kutokana na watanzania wengi kutotumia mahindi haya kama chakula ,hivyo kufuatia makubaliano tutakayoingia na Smart Group tutahamasisha wakulima kuanzia msimu huu Novemba walime kwa wingi kwa kuwa soko limepatikana” alisema Kusaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Smart Group ya Misri Yasser Attia alisema nchi inahitaji wa mahindi ya njano takribani tani milioni nane kwa mwaka ambayo kwa sasa zaidi wanaagiza toka Argentina na Ukraine.
Mwenyekiti huyo aliongeza kusema mwelekeo wa serikali ya Misri chini ya Rais Abdel Fattah el-Sisi ni kuona nchi hiyo inawekeza zaidi kwenye mataifa ya Afrika ndio maana wameamua kuja Tanzania kutafuta soko la mazao.
“Tumekuja Tanzania tukiamini ni ndugu zetu tunategemea kuongeza zaidi mahusiano ya kibiashara ili wakulima wa mahindi wazalishe zaidi na kupata faida kupitia ushirikiano huu na Misri “alisema Attia.
Attia aliongeza kusema nchi ya Misri ina uhitaji wa mazao mengi ya kilimo yakiwemo matunda kama parachichi, nanasi, papai, viungo, kahawa, korosho na chai hivyo watatazama ubora na gharama za usafirishaji mazao haya toka Tanzania hadi Misri kwa njia ya bandari ili waingie mikataba ya mashirikiano kwenye biashara.
Kampuni ya Smart Group ya Misri kupitia Mwenyekiti wake Yasser Attia imesema inahitaji mahindi ya njano kwa wingi toka Tanzania ili kutosheleza soko lao kwa ajili utengenezaji vyakula vya mifugo na samaki hivyo kuamua kuja Tanzania yenye ardhi nzuri na watu wenye kujituma kufanya kazi ikiwemo amani na utulivu.
Ikiwa Tanzania, ujumbe wa kampuni ya Smart Group watatembelea Dodoma, Zanzibar pamoja na Dar es Salaam kujionea na kuzungumza na watendaji wa serikali na sekta binafsi kuhusu ushirikiano wa kibishara kwenye sekta ya kilimo.
Imeelezwa kuwa Tanzania ina mahusiano ya kidiplomasia na nchi ya Misri kwa zaidi ya miaka 56 sasa hali inayopelekea mataifa haya kufanya biashara za kukuza uchumi ambapo Tanzania kupitia maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 hivi karibuni aliagiza Wizara ya Kilimo kutafuta masoko ya mazao ya wakulima .
“ Rais Dkt.John Pombe Magufuli ameelekeza wizara zetu zitafute masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, hivyo ujio wa wafanyabiashara toka Misri ni jitihada za wazi za kuwasaidia wakulima wa Tanzania kukuza uchumi wao na wa taifa jitihada ambazo tutaziendeleza pia kwa mazao mengine tofauti na mahindi ya njano “ alisema Kusaya.