Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini nchini kutumia masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini badala ya kutorosha madini kwani kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu uchumi wa nchi.
Profesa Kikula ameyasema hayo leo tarehe 23 Novemba, 2020 mjini Chunya Mkoani Mbeya kwenye mafunzo ya wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika mikoa ya kimadini ya Mbeya, Chunya na Songwe yenye lengo la kuwapa uelewa mpana kuhusu masuala ya usalama, afya, utunzaji wa mazingira na usafirishaji na matumizi sahihi ya baruti kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Alisema kuwa, katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wa madini wananufaika na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali kupitia Tume ya Madini imeanzisha masoko 38 na vituo vya ununuzi wa madini 39 na kuwataka kutumia masoko husika badala ya kuuza madini nje ya mfumo wa masoko.
“Kufanya biashara ya madini nje ya mfumo wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini ni kinyume na sheria, adhabu kali inatolewa ikiwa ni pamoja na utaifishaji wa madini pamoja na vyombo vya usafiri vilivyotumika kusafirisha madini husika, hivyo ninawasihi sana kutumia masoko ya madini pamoja na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa.
Akielezea mikakati ya Serikali kwenye utatuzi wa changamoto kwenye Sekta ya Madini, Profesa Kikula alisema kuwa Serikali imeanzisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na Maafisa Migodi Wakazi kwenye mikoa yote ili kusogeza huduma kwa wananchi pamoja na kufuta kodi nyingi ambazo zilikuwa ni kero kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Aliendelea kusema kuwa, pia elimu imekuwa ikitolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini hususan katika usimamizi wa mazingira ili kuhakikisha kuwa wanaendesha shughuli zao kwa usalama na kuepuka ajali mbalimbali huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini na kusisitiza kuwa mpaka sasa elimu imeshatolewa katika mikoa ya Singida, Katavi na Manyara na kuongeza kuwa yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ya kimadini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon Mayeka akizungumza katika mafunzo hayo aliwataka wachimbaji kutoa ushirikiano kwa Serikali kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwani Serikali imeazimia kuwainua wachimbaji wadogo wa madini.
Aliwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wachimbaji wadogo wa madini wasio waaminifu kwa kuuza madini nje ya mfumo wa masoko ya madini yaliyoanzishwa.
Wakati huohuo akizungumza katika mafunzo hayo, Mbunge wa Jimbo la Lupa Wilayani Chunya Mkoani Mbeya, Masache Kasaka alipongeza Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini kwa kuandaa mafunzo ambayo yatawapa uelewa mpana wachimbaji wadogo wa madini kuhusu namna bora ya kuendesha uchimbaji wa madini wenye kuzingatia usalama wa mazingira.
Alisema kuwa, kumekuwepo na changamoto kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wengi kuacha mashimo mara baada ya kumaliza shughuli za uchimbaji wa madini na kusababisha madhara kwa jamii inayozunguka.
Katika hatua nyingine alipongeza uanzishwaji wa Soko la Madini Chunya kwani wachimbaji wa madini wameanza kunufaika na shughuli za uchimbaji wa madini kupitia soko hilo.
Alitaja manufaa kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini kuuza madini yao kwa kufuata bei elekezi kwenye soko la dunia, usalama wakati wa biashara ya madini na kuzalisha ajira kwenye sekta nyingine.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wengine walioshiriki katika mafunzo hayo, Sailon Mpashila ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Makongolosi Wilayani Chunya mkoani Mbeya, mbali na kupongeza elimu bora iliyotolewa katika mafunzo hayo aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu katika mikoa mingine nchini.
“Wataalam kutoka Tume ya Madini wamefanya kazi nzuri sana ya kutuelimisha namna ya kuendesha shughuli zetu huku tukitunza mazingira, hii itapunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara,”alisema Mpashila.