KUSAYA : SERIKALI YAREJESHA MALI ZA BILIONI 61 KWA VYAMA VIKUU VYA USHIRIKA NYANZA,GEITA NA SIMIYU

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela ( kushoto) akikabidhi hati miliki 37 za mali zilizokuwa za vyama vikuu vya ushirika Nyanza,Geita na Simiyu kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) leo jijini Mwanza. Mali hizo zilizorejeshwa zina thamani ya shilingi Bilioni 61.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikabidhi hati miliki ( ) kwa mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Nyanza Bw. Benjamin Mikomangwa  (kulia) hafla iliyofanyika leo Mwanza. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikabidhi hati miliki(09) kwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Geita ( GCU)  Bibi Zainabu Mahenge (kulia) leo jijini Mwanza.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikabidhi hati miliki ( ) kwa mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Simiyu ( SIMCU) Bw. Emanuel Mboyi  (kulia) hafla iliyofanyika leo Mwanza. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella akiongea kwenye hafla ya kukabidhi mali za Vyama vikuu vya Ushirika vya Nyanza, Geita na Simiyu ambazo ziliporwa kinyume cha utaratibu kazi iliyofanywa na Timu Maalum Waziri Mkuu. Kulia ni Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya na kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emanuel Tutuba.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mali zilizokuwa za ushirika zilizorejeshwa serikalini leo jijini Mwanza ambapo julma ya hati 37 zenye thamani ya shilingi Bilioni 61 zimekabidhiwa tena kwa Nyanza, Geita na Simuyu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela (kushoto) akipokea hati miliki za ardhi,majengo na mitambo zilizorejeshwa kwa vyama vya ushirika toka kwa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu Bw. Asangye Bunga ( kulia) leo jijini Mwanza. Timu hiyo maalum iliundwa na Waziri Mkuu ikiwa ni agizo alilotoa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Agosti 2016.

Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella ( katikati)  na Katibu Mkuu Kilimo  Bw. Gerald Kusaya wakiwa na viongozi wa vyama vikuu vya ushirika vya Nyanza, Geita na Simiyu wakati wa hafla ya urejeshwaji mali za ushirika zilizorejeshwa kupitia Timu Maalum ya Waziri Mkuu.
( Habari na Picha na Wizara ya Kilimo

……………………………………………………………………………

Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kurejesha mali za vyama vikuu vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 61 zilizokuwa zikilikiwa kinyume cha utaratibu.

Akikabidhi hati 37 kwa wenyeviti wa vyama vya Nyanza (NCU),Geita (GCU) na Simiyu (SIMCU) leo (23.11.2020) jijini Mwanza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema kazi hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli aliyoyatoa mwezi Agosti mwaka 2016.

“ Leo nimekabidhi hati miliki 37 zinazojumuisha ardhi, majengo na mitambo yenye thamani ya shilingi Bilioni 61 zilizoporwa kinyemela na watu kutoka vyama vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu ambao ndio walikuwa wamiliki halali” alisema Kusaya.

Kusaya aliongeza kusema kazi hiyo ya kufuatilia na kurejesha mali imefanywa na Timu Maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2016 baada ya agizo la Rais Magufuli alipofanya ziara mkoani Mwanza kuwa mali zote za chama kikuu cha ushirika Nyanza zifuatiliwe na kurejeshwa toka kwa waliozimiliki kinyume cha utaratibu.

Ili kuhakikisha wanaushirika wananufaika na mali zao Katibu Mkuu Kusaya ametoa maagizo kwa viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuwa kurejeshwa kwa mali hizo zitumike kwa manufaa ya wakulima ambao ndio wamiliki.

Pili, Mrajis wa Ushirika nchini ahakikishe mali zilizorejeshwa zinakuwa salama na kuwa asitokee kiongozi yeyote atakayefanya ubadhirifu.

Tatu, kwa watu wote ambao bado wanamiliki zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu wazirejeshe mara moja kwa serikali kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa kupitia Timu Maalum ya Waziri Mkuu.

“ Nyanza kuna jengo lipo Nansio Ukerewe linaitwa Pamba Hostel imebainika mkataba wake na Saad Songolo ulikiukwa. Tunataka lirudishwe Serikalini, hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tunaomba uruhusu vyombo vya dola vifanye kazi yake ili mali hii ya wakulima irejeshwe” alisema Kusaya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela ametoa pongezi kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa uthubutu wao na uzalendo wa kutaka mali zote za wanashirika zilizochukuliwa kinyemela kurejeshwa kwa wamiliki ambao ni wakulima.

Mongela alisisitiza kuwa mkoa wa Mwanza tangu agizo lilipotolewa viwanja vya Furahisha tarehe 11 Agosti, 2016 umeshirikiana na Timu Maalum ya Waziri Mkuu kwenye ufuatiliaji na hatimaye kufanikiwa leo kurejesha mali hizi 27 za chama kikuu cha Nyanza na zingine za Simiyu na Geita.

“Leo tunamshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii hata kuagiza uchunguzi wa mali zao zilizoporwa na wajanja wachache kwenye ushirika” alisisitiza Mongela

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela alimpongeza Mwenyekiti wa kwanza wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu ambaye sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kwa kazi nzuri ya kufuatilia urejeshwaji mali hizo kazi iliyokamilisha na timu ya pili chini ya Asangye Bangu.

Aidha Mongela ametoa onyo kwa Viongozi wa Nyanza Cooperative Union kuwa wasimamie vizuri mali hizi ili zisije tena kuuzwa kwa watu kinyume cha utaratibu  na kuwa sasa Nyanza inatakiwa kuwa na Mtendaji Mkuu mwenye weledi na ujuzi wa kusimamia ushirika.

Mongela ameiomba wizara ya kilimo “ ifanye kazi ya kuhakikisha vyama vikuu vya ushirika vinapata na kuajili mameneja wakuu wenye weledi, taaluma, ujuzi na uadilifu kuongoza ushirika ili vijiendeshe kibiashara badala ya kutumia uzoefu tu usio na tija” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Akiwasilisha taarifa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu Asangye  Bangu alisema mali hizo zilizorejeshwa ni sehemu ya zoezi endelevu la kufuatilia watu wote waliojimilikisha au kuuziwa zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu. 

Bangu alitaja mali zilizorejeshwa kwa vyama vikuu vya ushirika Nyanza kuwa ni 27, Geita 9 na Simiyu 2 zikiwamo viwanja, majengo na mitambo na kuwa timu yake inaendelea kufuatilia mali zingine kwenye vyama hivi na vingine ikiwemo Kilimanjaro( KNCU) Shinyanga (Shirecu) na maeneo mengine.

Akitoa shukrai kwa niaba ya wanaushirika nchini Mrajis wa Ushirika Dkt. Benson Ndiege alisema kurudishwa kwa  mali za ushirika kutasaidia kufufua na kuimarisha utendaji kazi wa vyama vya ushirika nchini.

Dkt. Ndiege alisema atahakikisha mali zilizorejeshwa zinatumika kwa manufaa ya wakulima ili ziwasaidie kuondokana na umasikini wa kipato .

.

Mwisho

Imetolewa na;

 Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MWANZA

23.11.2020

Post a Comment

Previous Post Next Post