TUMIENI FEDHA ZA WAFADHILI KUENDELEZA KILIMO SHAMBANI- KUSAYA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akizungumza kwenye kongamano la kilimo mseto wakati wa maonesho yaliyofanyika jana Musoma chini ya uratibu wa shirika la Vi Agroforestry.

Meneja Mradi  Vi Agroforestry Tanzania Bw.Kent Larsson akitoa shukrani kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo mara baada  ya kufungua maonesho ya kilimo mseto jana mjini Musoma. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya.  

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) jana mara baada ya mazungumzo yao Ofisini kwa Mkuu huyo wa Mkoa mjini Musoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akihutubia wakulima wakati alipofungua maonesho ya siku tatu ya kilimo mseto mjini Musoma jana.

Mkurugenzi wa Shirika la Vi Agroforestry Bw. Thadeus Mbowe akizingumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya kilimo mseto jana mjini Musoma yaliyoandaliwa na shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika wenza na kushirikisha wakulima na wajasiliamali toka mikoa ya Mara, Mwanza,Dodoma, Rukwa, Dar es Salaam, Tabora na Kagera.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akipiga ngoma ya jadi wakati alipofungua maonesho ya kilimo mseto mjini Musoma jana. 
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo

……………………………………………………………………………….

Serikali imezitaka taasisi na mashirika binafsi yanayopokea fedha toka kwa wahisani na wafadhili hususan kutoka nje ya nchi kuzitumia katika miradi inayokuza sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima kupata kipato.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa jana (19.11.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofungua maonesho ya siku tatu ya kilimo mseto yanayofanyika Musoma mkoani Mara kwa uratibu wa shirika la Vi Agroforestry na mshirika wenza.

“ Hizo fedha mnazopewa kuendesha shughuli za taasisi zenu zitumieni vizuri na kuepuka matumizi mabaya ili wafadhili waendelee kuiamini Tanzania na wakulima wanufaike badala ya watu binasfi kujinufaisha” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema yapo mashirika na taasisi hapa nchini ambayo yanapokea fedha toka kwa wahisani na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuendesha shughuli za kilimo lakini hawatimizi wajibu wao na kuharibu taswira ya nchi kwani wakulima hawanufaiki.

“ Sipendi kuja kuona nafanya uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha kwenye taasisi au mashirika yanayojihusisha na miradi ya kilimo hapa nchini, hivyo nawasihi tumieni fedha mnazoletewa na wahisani kuendeleza mashamba ya wakulima badala ya kujinufaisha wenyewe kwa posho zisizo halali” alionya Kusaya.

Kusaya alionyesha kukerwa na tabia iliyojengeka kwa baadhi ya mashirika kutumia fedha nyingi kwenye makongamano (capacity building) badala ya ufanyaji kazi mashambani ili wakulima wapate elimu na teknolojia ikiwemo mbegu bora na huduma za ugani kuwafanya wazalishe mazao bora.

Kusaya alibainisha kuwa Tanzania ina eneo linalofaa kwa kilimo hekta milioni 44 sawa na asilimia 46 ya ardhi yote huku eneo linalolimwa kwa sasa ni hekta milioni 10.8 sawa na asilimia 24 hivyo kuhitaji wawekezaji wengi wenye mitaji na teknolojia .

Aliongeza kuwasihi watendaji wa mashirika na taasisi zinazofanya kazi kwenye sekta ya kilimo nchini kuacha kurudia rudia kazi badala yake wawe na utaratibu wa kugawana maeneo ya kuhudumia wakulima kote nchini badala ya kulenga eneo moja la nchi.

“ Msipende kurudia rudia shughuli na miradi ambayo tayari imetelekezwa na mashirika au taasisi nyingine na tambueni kuwa ninyi ni watanzania kwa kuwa wazalendo ili wakulima wanufaike na fedha za miradi ” alisisitiza Kusaya.

Kusaya ametoa wito kwa wadau ikiwemo shirika la Vi Agroforestry kuwasilisha serikalini mpango wa kuboresha sera ya taifa ya kilimo ili kuingiza suala la kilimo mseto ambapo wizara za kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na utalii zitashirikishwa kwa karibu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Vi Agroforestry Thadeus Mbowe alitoa ombi kwa wizara ya kilimo kuchukua hatua za kuhuisha na kutunga sera ya taifa ya kilimo mseto ili iwezeshe wadau wengi kufanya kazi kwenye mikoa yote nchini.

Mbowe alisema uwepo wa sera ya taifa ya kilimo mseto utakuza sekta hii kuifanya kuwa endelevu na kuchangia zaidi katika upatikanaji wa chakula na kipato cha mkulima.

Aidha, aliongeza kusema maonesho ya kilimo mseto yanafanyika Musoma yakilenga kuhamasisha wakulima kutambua na kupata elimu ya namna ya kupunguza mabadiliko ta tabia nchi ili kuendeleza kilimo chenye tija.

“Tunapendekeza Wizara ya Kilimo itoe msukumo kwenye kuanzishwa sera ta taifa ya kilimo mseto na kuwezesha utafiti wa mbegu bora na visumbufu vya mazao ili wakulima wawe na uhakika zaidi wa kufanya kilimo biashara” alisema Mbowe.

Shirika la Vi Agroferestry kwa ushirikiano na mashirika wenza wameandaa maonesho ya siku tatu ya kilimo mseto yaliyoshirikisha wakulima, wajasiliamali, wataalam wa teknolojia za kilimo toka mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Tabora, Dodoma, Dar es Salaam na Rukwa ambapo bidhaa mbalimbali za kilimo zinaonyeshwa kwa wakulima.

Post a Comment

Previous Post Next Post