Katibu mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kikao kazi maalumu kilichowakutanisha na Wahariri wa habari nchini amesema kuwa Wizara hiyo imejipanga katika kuhakikisha pato la taifa na wavuvi linaongezeka kupitia sekta hiyo, Leo jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa mradi wa SWIOfish Dkt. Nichrous Mlalila akitoa mada katika kikazi hicho kilichowakutaanisha na Wahariri na Waandishi wa habari nchini, leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahariri na Waaandishi wa habari wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika kikao kazi hicho kilichowakutanisha na Katibu mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Leo jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa mradi wa SWIOfish, Dkt. Nichrous Mlalila (kulia,) akifafanua jambo wakati wa kikao kazi hicho kilichowakutanisha na Wahariri na Waandishi wa habari, leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Kaiza Mutagwaba akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari katika kikao kazi maalumu kilichowakutanisha na Wizara hiyo, leo jiojini Dar es Salaam.
Mjadala ukiendelea.
Katibu mkuu Uvuvi wa Wizara ya ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiwa katika picha ya pamoja na Wahariri na Waandishi wa habari nchini mara baada ya kikao kazi hicho ambacho ameeleza mipango, mikakati na mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa SWIOfish, leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KATIBU Mkuu Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amekutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini na kueleza utekelezaji wa wa mradi wa SWIOfish ambao ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uvuvi ya 2015, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2015/16-2020/21) na programu ya kuendeleza sekta ya uvuvi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari nchini wakati akifungua kikao kazi hicho jijini Dar es Salaam leo, Dkt. Tamatamah amesema kuwa Mradi huo wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH,) unatekelezwa kwa kipindi cha miaka 6 na kufadhiliwa na na Benki ya dunia kwa thamani ya dola za kimarekani milioni 36 na ulianza Juni 22, 2015 na utafikia tamati Septemba 21, 2021.
"Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha usimamizi madhubuti wa uvuvi katika ngazi za jamii, taifa na kimataifa na malengo mengine ni kujenga uwezo kwa nchi katika kusimamia rasilimali za uvuvi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi wa bahari kuu na hiyo ni pamoja na kuinua uchumi wa jamii ya watu wa Pwani na pato la Taifa kwa ujumla kupitia rasilimali za uvuvi." Amesema.
Dkt. Tamatamah amesema kuwa tangu mradi huo uanze mwaka 2016 umeonesha mafanikio chanya na una mwelekeo mzuri wa kiutekelezaji ikiwemo kuzuia matumizi ya baruti na mabomu katika uvuaji kwa asilimia 100 na hiyo ni kutokana na kuimarishwa kwa doria pamoja na kuongezeka kwa uelewa kwa jamii ya Pwani kuhusu madhara ya Uvuvi haramu.
"Wizara ipo makini sana, usajili wa vyombo vya Uvuvi umeongezeka mara dufu hadi kufikia asilimia 58 kutoka asilimia 25 ya awali kabla ya mradi....Tutaendelea kutoa mafunzo endelevu katika sekta hii ili kuweza kuiboresha zaidi." Ameeleza.