*************************************
NA FARIDA SAIDY, MOROGORO.
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuhakikisha wanabuni na kutekeleza mikakati ya kuongeza na kukuza wigo wa mazao ya utalii ili kuongeza idadi ya ya watalii kutoka 1,510,151 mwaka 2019/2020 hadi kufikia watalii 5,000,000 ifikapo mwaka 2025/2026.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Aloyce Nzuka wakati akifunga kikao kazi kilichowakutanisha Manaibu Kamishina wa TAWA, Makamishna Wasaidizi Waandamizi, Wakuu wa Vituo pamoja na Maafisa wengine wa TAWA, ambapo amesema ili kufikia malengo hayo TAWA inajukumu la kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii.
Aidha Katibu Mkuu huyo amesema kufuatia mlipuko wa virus vya korona vilivyoathiri sekta ya utalii duniani Wizara imejipanga kuongeza mapato bila ya kuathiri uhifadhi, ambapo imerekebisha kanuni kadhaa na kutunga kanuni mpya ikiwemo kuongeza muda wa kuwinda bila ya kubadilisha mgao wa wanyama.
Kanuni nyingine ni kuongeza muda wa kumiliki vitalu hadi mwaka 2022,kuruhusu kushiriki kwenye mnada wa vitalu bila ya kuhitajika kusajili kampuni kabla ya mnada, kufanya mapitio ya kanuni za uwindaji na kutunga kanuni za kuwezesha uwekezaji mahiri.
Pia Katibu Mkuu ameiagiza TAWA kuandaa andiko na kutengeneza video ambayo itawasilishwa kwa Mabalozi wa Tanzania walioko nchi mbalimbali ili wasaidie kutangaza uwindaji wa kitalii.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Uhifadhi (TAWA) Bwana Mabula Misungwi amesema Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori nchini (TAWA) imejipanga kudhibiti ujangili ndani na nje ya mapori ya akiba na mapori tengefu pamoja na kusimamia shughuli za uwindaji wa wanyamapori zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mamlaka hiyo lakini pia mamlaka imesema inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mishahara midogo kwa watumishi na uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kibinaadamu, jambo ambalo linachangia baadhi ya watumishi kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa.
Hata hivyo amesema katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na nidhamu na maadili ya kazi mamlaka imekuwa ikuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matukio ya watumishi kujihusisha na vitendo vya rushwa na ujangili.