Na Amiri Kilagalila,Njombe
Mratibu wa uchaguzi mkoa wa Njombe bwana Hilmar Danda amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi za jimbo na kata kwenda kusimamia uchaguzi wa Oktoba 28 Mwaka huu kwa kufuata sheria za uchaguzi.
Bwana Danda ametoa agizo hilo wakati wa kuwaapisha wasimamizi wasaidizi hao katika jimbo la Lupembe zoezi lililoambatana na semina ya namna ya kwenda kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba wasipozingatia sheria za uchaguzi wanaweza kujikuta pabaya.
"Mkazingatie sheria,kanuni na maelekezo mnayopewa kutoka tume ili mwisho wa siku muweze kuitendea haki tume"alisema Danda
Akitoa mafunzo hayo afisa wa uchaguzi katika jimbo la Lupembe Bwana Sifa Faramagoha anasema mbali na kutakiwa kuzingatia sheria wakati wa zoezi hilo lakini wanapaswa kuwasikiliza na kuwasaidia wapiga kura pale watakapokuwa wanahitaji msaada.
Naye msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Lupembe Bwana Ally Juma ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Njombe wakati akiwaapisha wasimamizi wasaidizi hao amesema semina hiyo ya siku mbili imelenga kuwaelekeza shughuli nzima itakayofanyika katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu na mambo wanayotakiwa kuyafanya.
"Tunawapa semina hii ili kujua mambo mbali mbali na kuwajengea uwezo ili siku hiyo zoezi la uchaguzi liweze kuwa la haki na usawa ili uchaguzi pia uweze kuwa wa huru na haki"alisema Ally Juma Ally
Msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Lupembe Bwana Ally Juma akitoa maelezo kwa wasimamizi wa uchaguzi mapema hii leo kabla ya zoezi la kuwaapisha.Wasimamizi wa uchaguzi jimbo la upembe wakisikiliza maelekezo wakati wa semina ya uchaguzi ya siku mbili kutoka tume uliofanyika ukumbi wa shule ya sekondari Mtwango.Wasimamizi wa uchaguzi Jimbo la Lupembe wakisaini viapo vyao mara baada ya kuapishwa na Msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Lupembe Bwana Ally Juma