TANZANIA NA UJERUMANI KUENDELEZA USHIRIKIANO KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU

 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo  akizungumza  na wawakilishi kutoka ubalozi wa Ujerumani (hawapo pichani) wakati walipotembelea ofisi za Wizara jijini Dodoma
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Maendeleo katika Ubalozi wa Ujerumani Dkt. Katrin Bornemann akizungumza wakati wa kikao cha pamoja na Wizara ya Elimu kilichofanyika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja  na wawakilishi kutoka  Ujerumani mara baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiteta jambo na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Maendeleo katika Ubalozi wa Ujerumani Dkt. Katrin Bornemann mara baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika ofisi za Wizara Mtumba - Dodoma.

SERIKALI ya Tanzania na Ujerumani wamekubalina kuendeleza mashirikiano kwenye elimu  ya juu, Ufundi na Msingi ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata ujuzi wa kuweza kushiriki katika ujenzi wa Taifa. 

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wawakilishi kutoka ubalozi wa Ujerumani na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika katika Ofisi za wizara Jijini Dodoma Katibu Mkuu Dkt Leonard Akwilapo amesema kwa sasa nchi inatekeleza miradi  mikubwa ya ujenzi hivyo kuna  uhitaji wa wataalamu wenye ujuzi katika eneo.

“Tunajenga reli ya kisasa ya umeme SGR, madaraja na ipo miradi mingine mikubwa inatekelezwa, pamoja na kwamba tunao wataalamu wetu nchini bado tunahitaji wajiendeleze ili kupata ujuzi zaidi. Kwa hiyo tumezungumza nao kuona ni namna gani tunaweza kushirikiana kuwezesha mafunzo  kwa Vijana  hapa nchini na hata nchini kwao,” aliongeza Dkt. Akwilapo.

Akizungumzia uimarishaji wa elimu ya Msingi Katibu Mkuu Akwilapo amesema wamekubaliana kushirikiana  kuongeza ujuzi wa walimu katika mbinu mpya za ufundishaji ikiwa ni pamoja na  kutoa vifaa vya kufundishia.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Maendeleo katika Ubalozi wa Ujerumani nchini Dkt. Katrin Bornemann amesema Serikali ya Ujerumani itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu ambao wamekuwa nao katika elimu ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanaendelea kupata Elimu bora.

Ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa muda mrefu kuanzia miaka ya 80 na 90 ambapo kupitia shirika lake la DAAD  waliweza kutoa ufadhili wa masimo kwa  wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Post a Comment

Previous Post Next Post