MKUTANO KATI YA MENEJIMENTI YA WIZARA NA UJUMBE KUTOKA UBALOZI WA AFRIKA KUSINI NCHINI TANZANIA.

 

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu (wa kwanza kushoto) akizungumza wakati wa kikao na Kaimu balozi wa Afrika ya Kusini, ndugu Sizwe Mayoli walipokutana leo tarehe 24 Septemba, 2020 katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kushoto ni ndugu Dumo Siyotula katibu wa siasa wa ubalozi wa Afrika ya kusini.

Baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki kikao hicho. 

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu (kushoto) akizungumza na Kaimu balozi wa Afrika ya Kusini, ndugu Sizwe Mayoli wakati wa kikao cha kujadili Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano katika Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

********************************************

Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu leo tarehe 24 Septemba, 2020 amekutana na ujumbe kutoka Ubalozi wa Afrika ya kusini nchini Tanzania katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Akiongea na ugeni huo, ndugu Ally Gugu alisema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa kwenye ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kwa muda mrefu tangu kipindi cha kudai uhuru. Hivyo ni jambo jema kushirikiana katika kuendeleza biashara kati ya nchi hizo mbili.

Alisema ushirikiano huo umezidi kuimarika kwa uwepo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo nchi hizi mbili zilikubaliana kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano katika Sekta ya Viwanda na Biashara. Lengo la MoU hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara zaidi kwa kuongeza biashara (trade volume) kwa maslahi ya pande zote mbili ukizingatia Afrika ya Kusini ni moja ya nchi iliyokinara katika uwekezaji barani Afrika.

Naye Kaimu balozi wa Afrika ya Kusini, ndugu Sizwe Mayoli amesema kuwa amefurahi kupata fursa ya kujadili masuala ya ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Afrika ya Kusini katika kikao hicho.
Aidha, baadhi ya masuala yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (MoU) ya Ushirikiano katika Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. MoU hiyo inatoa fursa ya kuunda Kamati ya Pamoja ya Biashara na Uwekezaji ktika nchi hizi mbili.

Pia kikao hiki kimehitimishwa kwa pande zote mbili kuunda kamati ya pamoja itakayoshirikisha wajumbe kutoka Tanzania na Afrika ya Kusini ili kushirikiana pamoja katika kutekeleza Hati ya makubaliano (MoU) katika sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Post a Comment

Previous Post Next Post