MATOKEO YA KAZI YETU NI WANANCHI KUPATA HUDUMA YA MAJI- MHANDISI KEMIKIMBA

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (katikati) akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wawezeshaji watakaozijengea uwezo bodi za wakurugenzi wa mamlaka za maji nchini katika masuala ya menejimenti. Mafunzo yamefanyika katika ukumbi wa DUWASA jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji, Mhandisi Charles Mafie na Mwezeshaji Mhandisi Alex Kaaya (kushoto).

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji, Mhandisi Charles Mafie akiongea na wataalam wa sekta ya maji kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (kushoto) kufungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa Sekta ya Maji yaliyofanyika ukumbi wa DUWASA jijini Dodoma leo.

Mwezeshaji Mhandisi Alex Kaaya akitoa mafunzo kuhusu menejimenti hususan katika mamlaka za maji nchini ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (katikati) katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa Sekta ya Maji baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika ukumbi wa DUWASA jijini Dodoma leo.

**********************************

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewataka watendaji katika sekta ya maji nchini kuhakikisha matokeo ya kazi zao ni wananchi kupata huduma ya maji ya uhakika.

Mhandisi Kemikimba amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akishiriki mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa sekta ya maji atakaofanya kazi ya kuzijengea uwezo bodi za wakurugenzi wa mamlaka za maji hasa katika menejimenti ya mamlaka hizo.

 “Mhakikishe mafunzo mtakayoyatoa kwa bodi za wakurugenzi wa mamlaka za maji nchini yanasaidia kufikia malengo ya sekta yetu ya maji na ya kitaifa kwa kuwapatia wananchi huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza” Mhandisi Kemikimba amesema. 

Aidha, amewashauri washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia suala la    Ufuatiliaji na Tathmini katika ufundishaji wao ili hatimaye serikali iweze kujua huduma ya maji kwa wananchi inapatikana  kwa kiwango gani katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mhandisi Kemikimba amesema kuongea lugha moja katika huduma ya maji ni jambo la msingi, hivyo ni muhimu kujua wananchi wanapokeaje huduma hiyo na mrejesho wao unafanyiwa kazi kwa haraka.

Mamlaka za maji ni matokeo ya mabadiliko yaliyofanywa na serikali miaka ya 90 ambapo zilikasimiwa madaraka ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post