MABANDA YA TGC NA MRI YAENDELEA KUNG'ARA KWENYE MAONESHO YA MADINI GEITA

 


Mbanda ya Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI) yameendelea kuwa kivutio katika Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea katika Uwanja wa Kituo cha Uwekezaji wa Bombambili mjini Geita.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa mkoa wa Geita na mikoa ya jirani wamesema kuwa, wamefurahishwa na huduma nzuri zinazotolewa na Kituo cha Jemolojia Tanzania kwani awali walikuwa hawana mwanga wa miamba kutengeneza bidhaa ambazo zinaweza kutumika kama urembo sehemu mbalimbali.

Akizungumza na wananchi hao, Mjiolojia Jumanne Shimba wa TGC amesema kuwa, lengo  la ushiriki katika maonesho hayo ni kutoa elimu juu ya uongezaji thamani madini ili kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali za madini kwa wananchi na Taifa.

Akielezea fursa zinazopatikana katika kituo hicho, Shimba ameeleza kuwa kituo kinatoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa kozi mbalimbali zinazohusu uongezaji thamani madini kwa wananchi hususan wafanyabiashara wadogo.

Katika hatua nyingine Shimba amewakaribisha wananchi hususan vijana kujiunga na kozi mbalimbali katika kituo hicho ili kuweza kujiajiri na kujiingizia kipato huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Naye mkufunzi kutoka Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Mohamed Ngido amesema kuwa chuo hicho kinatoa kozi mbalimbali katika ngazi ya cheti, diploma na mafunzo ya muda mfupi.

Amesema lengo la mafunzo ni kuzalisha wataalam wa madini nchini ili wawe sehemu ya umiliki wa uchumi wa madini nchini.

"Tuna mpango wa kuhakikisha tunatoa elimu bora hususan katika kada ya madini kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wa juu ili waweze kuendesha shughuli za uchimbaji madini kitaalam bila kuathiri mazingira," amesema Ngido

Aidha Ngido amepongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa mikakati thabiti iliyowekwa katika kukiwezesha chuo hicho ili kutoa huduma bora na kuwawezesha wadau wa madini kuongeza uzalishaji wa madini kutokana na elimu wanayoipata.

Post a Comment

Previous Post Next Post