WATAFITI TUMIENI NJIA RAFIKI KUDHIBITI VISUMBUFU VYA MIMEA KIBAIOLOJIA- KUSAYA

  Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akipata maelezo ya namna watafiti wanavyozalisha z mbegu bora za zao la viazi leo alipotembelea kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Kibaha.

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mbegu bora ya miwa wakati alipotembelea kituo cha Utafiti wa Miwa (TARI) Kibaha. Kulia ni Meneja wa Kituo hicho Dkt.Hildelitha Msita. Kituo hico kimefanikiwa kuzalisha mbegu bora za miwa ,muhogo na viazi aina 26 .

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kulia) akitazama mche wa mbegu ya muhogo unaozalishwa na Kituo cha Utafiti TARI Kibaha leo alipotembelea kukagua utendaji kazi wa kituo hicho.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akipanda mti wa kumbukumbu wakati wa ziara yake kukagua utendaji kazi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kibaha. 

(Picha na Habari na Wizara ya Kilimo)

***********************************

Wizara ya Kilimo imesema itaendelea kuhakikisha visumbufu vya mimea kwenye mazao ya wakulima vinadhibitibitiwa kwa kupitia ujenzi wa maabara bora itakayojengwa Kibaha.

 

Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo (24.08.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipofanya ziara ya kikazi kukagua kituo cha Kudhibiti Visumbufu vya Mimea Kibaolojia kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani.

 

“Wizara imejipanga kuhakikisha visumbufu vya mimea vinapatiwa suluhu ili kusaidia wakulima kuwa na mazao bora pasipo kuharibiwa na wadudu vamizi kwa kujenga maabara bora na yakisasa kupitia mradi wa Kudhibiti
Sumukuvu” alisema Kusaya.

 

Kusaya aliwataka watafiti wanaofanya kazi kwenye kituo hichio kuhakikisha wanatumia njia rafiki katika kudhibiti visumbufu vya mimea kuliko matumizi ya kemikali ili kumlinda mlaji wa mazao ya kilimo.

 

Kadhalika amekiagiza kituo hicho kufanya utafiti utakaopunguza matumizi ya viuatilifu vyenye sumu (synthetic insecticide) hapa nchini ili kulinda afya
za wazalishaji,walaji na mazingira kwa kutumia njia na teknolojia rafiki kwa mazingira.

 

Aliongeza kusema wizara yake inatambua umuhimu wa utafiti kwenye
Kilimo ndio maana kupitia mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) wizara imepanga kuanza ujenzi wa maabara bora ya Kilimo ambayo itakuwa ya kimataifa katika kupata suluhu ya visumbufu vya mimea.

 

“Tunao mradi mkubwa wa kudhibiti sumukuvu chini ya serikali ya awamu ya tano ambao utasaidia kituo cha udhibiti wa vumbufu vya mimea kibaolojia kuwa na karantini ya kimataifa hapa Kibaha utakapokamilika
mwaka 2021” alisisitiza Katibu Mkuu Kusaya.

 

Naye Mratibu wa mradi wa Kudhibiti Sumukuvu( TANIPAC) Clepin Josephat alieleza kuwa kuamilika kwa karantini hiyo kutasaidia kuboresha utafiti unaofanywa katika udhibiti wa visumbufu vya mimea na utanatarijwa kugharimu bilioni mbili utakapokamilika mwaka 2021.

 

Akizungumzia kituo hicho, Afisa Mfawidhi Kituo cha Kudhibiti Visumbufu vya Mimea Kibailojia cha Kibaha Nsami Elibariki alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1990 baada ya kutokea mdudu vamizi kidung”ata wa
muhogo (cassava mealybug) ambaye alisababisha kuwa na ukosefu mkubwa wa chakula kwenye maeneo yote yalimwayo muhogo nchini.

 

 Elibariki alitaja mafanikio ya kituo hicho kuwa ni pamoja na udhibiti wa kidugata wa mhogo, utitiri wa muhogo, udhibiti wa funza wa mabua, udhibiti wa nzi mweupe na pia udhibiti wa magugu maji .

 

Katika hatua nyingine Kusaya alitembelea Kituo cha Utafiti wa Zao la Miwa (TARI) Kibaha na kukagua utendaji kazi wake ambapo amejionea kazi nzuri inayofanyika kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa sukari.

 

Kusaya alisema takwimu za mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 470,000 wakati uzalishaji ndani umefikia tani 350,000 hivyo kuwa na upungufu unaosababisha serikali itumie fedha nyingi kuagiza sukari nje.

 

Aliongeza kusema watafiti wa zao la sukari chini ya TARI Kibaha wanatakiwa kuhakikisha wanapata jawabu la kwanini tatizo la upungufu wa sukari linaendelea kuwepo nchini.

 

“ Watafiti mna jukumu la kuhakikisha tunapata jawabu la kumaliza upungufu wa sukari.Hili ni deni kubwa kwa taifa, fanyeni utafiti wa mbegu bora za miwa zenye kutoa mazao mengi na zenye kuhimili magonjwa” aliagiza Katibu Mkuu Kusaya.

 

Akizungumza kwa niaba ya watafiti Dkt Luambano Nessie alisema wanaiomba serikali itoe motisha kwa watafiti ikiwepo vitendea kazi kama magari ambavyo vitasaidia kuboresha utendaji kazi.

 

“Tunafanya kazi hadi saa 5 usiku lakini hatupati posho na pia usafiri wa kuturudisha usiku ni tatizo pamoja na nyumba hazitoshi .Hili linatupa shida” alisema Dkt.Luambano.

 

Pamoja na mazingira magumu ya kazi za utafiti Katibu Mkuu huyo ameahidi kukipatia kituo cha TARI Kibaha trekta moja na vifaa bora vya maabara kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za miwa na
kuzisambaza nchini.

 

“Tunataka kuona kazi za utafiti zikiendelea licha ya changamoto kwa kuwa lengo la serikali ni kuona mazao ya wakulima yanazalishwa zaidi na kuwa nchi inajitosheleza kwa uzalishaji wa sukari “alisema Kusaya.

 

Sambamba na uwepo wa changamoto za vituo vya utafiti nchini, Kusaya alisema wizara itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi ikiwemo maslahi yao,upatikanaji wa vifaa na fursa za mafunzo .

 

“ Napenda maendeleo ya watumishi hivyo nawasihi kopeni fedha kutoka mfuko wa Hazina na pia Mfuko wa Pembejeo unaotoa riba nafuu sana ili mjiendeleze kimaisha na kuwa na uhakika wa kipato kabla ya kustaafu” alisema Kusaya na kuongeza kuwa anapenda kuona watumishi wakiwa na
furaha mahala pa kazi.

 

Katibu Mkuu huyo yupo kwenye ziara ya kikazi ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara ya Kilimo kuona utendaji kazi wake na kuzungumza na watumishi ili wafanye kazi kwa bidii na kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini

Post a Comment

Previous Post Next Post