NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetangaza maboresho makubwa ya mfumo wake wa usajili yanayowezesha wananchi kupata huduma nyingi kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na usalama katika urasimishaji wa biashara nchini.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Mzunguni jijini Dodoma, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuph Mwasakafyuka Regio, alisema mfumo huo mpya umeondoa changamoto zilizokuwapo kwenye mfumo wa awali wa ORS na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja.
Alisema kupitia mfumo huo, huduma ambazo awali zilihitaji mteja kufika ofisini sasa zinaweza kufanyika mtandaoni, ikiwemo uwasilishaji wa taarifa za dhamana (charges) zinazohusisha mikopo kutoka taasisi za fedha.
Regio alieleza kuwa mfumo huo pia umeongeza uwazi kwa kuwawezesha wananchi kupata taarifa za kampuni kwa urahisi zaidi, ikiwemo hali ya uwasilishaji wa taarifa za mwaka (annual returns), pamoja na kuimarisha usalama wa taarifa kwa kuwajulisha wanahisa na wakurugenzi kila mabadiliko yanapofanyika ndani ya kampuni.
Alisema ili kutumia mfumo huo, mwananchi anatakiwa kuwa na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN), namba ya simu inayotumika na anuani sahihi ya barua pepe.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara, wakulima na wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la BRELA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Viwanda na Biashara ili kujifunza matumizi ya mfumo huo na kupata huduma mbalimbali za urasimishaji wa biashara.
BRELA inaendelea kutoa huduma za usajili wa majina ya biashara, makampuni, leseni za biashara Kundi A, leseni za viwanda na usajili wa awali wa alama za biashara, huku ikisisitiza kuwa urasimishaji wa biashara ni hatua muhimu katika kukuza uchumi na kuongeza fursa za biashara.
