TUMEWEKEZA NGUVU KUBWA KUTANGAZA VIVUTIO VYA TANZANIA NCHI ZA ULAYA -BALOZI MNDEME

Na Hamis Dambaya,Stockholm 

Balozi wa Tanzania nchini Sweden mheshimiwa Swahiba Mndeme amesema miongoni mwa kazi kubwa waliyonayo katika Ubalozi huo ni kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika nchi ya Sweden, Finland, Norway, Denmark, Iceland, Latvia, Lithuania, Estonia na Ukraine ili kuongeza idadi ya watalii kutoka nchi hizo kutembelea Tanzania.

Balozi Mndeme ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na maafisa kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliotembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini  Sweden kushiriki programu mbalimbali ikiwemo siku ya tamasha la Kiswahili kwa lengo la kunadi vivutio vya utalii 

“Maeneo ninayoyasimamia ya takriban nchi tisa ni ya kimkakati hivyo mimi na watumishi wenzangu katika ubalozi wetu, tunatumia fursa zilizopo katika nchi hizi  kutangaza vivutio vyetu na ninaamini tukishirikiana kwa pamoja tutaibua soko jipya la utalii katika ukanda huu”,alisema balozi Mndeme.

Kwa upande wake Meneja mawasiliano na uhusiano kwa umma wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Hamis Dambaya amesema Mamlaka ina mkakati wa kuibua mazao mapya ya utalii ikiwemo ya malikale, urithi utamaduni na kuendeleza mazao yaliyopo ili kuyaongezea thamani kwa wageni wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro.

“Tuna kampeni mbalimbali tunazoziendesha ikiwemo kuhamasisha watu duniani kurudi nyumbani Ngorongoro ili kupata ukweli kuhusu historia ya binadamu wa kale aliyepatikana katika eneo la Ngorongoro”,alisema bwana Dambaya.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatangaza shughuli zake za utalii nchini Sweden ambapo itashiriki katika tukio kubwa la maadhimisho ya siku ya kiswahili nchini humo.


Post a Comment

Previous Post Next Post