Mwandishi Wetu,
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayosimamia na kuratibu maendeleo ya kilimo hai Tanzania (TOAM), Bakari Mongo, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya mbolea hai kwa wakulima na wadau nchini.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TFRA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka pamoja na juhudi zake za kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea, ikiwemo mbolea hai.
Mongo amesema kuwa jitihada za TFRA katika kutoa elimu kuhusu matumizi ya mbolea hai ni muhimu katika kukuza kilimo endelevu, kulinda afya ya udongo na kuongeza uelewa wa wakulima na wadau kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.
Kwa upande wake, Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya, amesema kuwa utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya Mamlaka, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbolea hai.
Wadau, wakulima na viongozi mbalimbali wanaendelea kutembelea banda la TFRA ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Mamlaka, majukumu yake pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana katika tasnia ya mbolea.





