Mwandishi Wetu,
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Prof. Tumaini Nagu, amezielekeza Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa na Halmashauri kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, usimamizi wa rasilimali na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi sahihi.
Prof. Nagu ametoa maelekezo hayo leo Julai 29, 2026, wakati akifungua Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa, Waratibu wa Huduma za Maabara, Wafamasia na Waratibu wa Huduma za UKIMWI unaofanyika jijini Dodoma. Amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika usimikaji wa Mfumo wa GoTHOMIS ambapo vituo 7,591 kati ya 7,889 vya afya ya msingi ambavyo ni sawa na asilimia 52 tayari vimeunganishwa na mfumo huo, huku akisisitiza kuongeza kiwango cha matumizi yake.
"Ninawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha matumizi ya mifumo ya kidijitali hususan GoTHOMIS yanaimarishwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya. Hakikisheni mfumo huu unatumiwa katika usajili wa wagonjwa, huduma za maabara, famasi, mionzi na maeneo mengine yote muhimu. Vilevile, hakikisheni mapato yote ya huduma za afya yanakusanywa kupitia Mfumo wa Serikali wa Malipo kwa Njia ya Kielektroniki (GePG) kwa kuzingatia taratibu za Serikali," amesema Prof. Nagu.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika sekta ya afya kwa kuongeza matumizi ya GePG, ambao tayari unatumika katika vituo 6,779 kati ya 7,889 vya kutolea huduma za afya ya msingi sawa na asilimia 85, huku akisisitiza pia kuongeza matumizi ya NHIF Portal ili kurahisisha uwasilishaji wa madai, kupunguza ucheleweshaji wa malipo na kuimarisha usimamizi wa mapato ya vituo vya afya.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka OWM-TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amesema miongoni mwa malengo ya mkutano huo ni kupitia utekelezaji wa majukumu ya Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa (RCHMT), pamoja na kujadili matumizi ya mifumo ya kidijitali ikiwemo GoTHOMIS, JPH na mifumo mingine ili kuendelea kuboresha huduma jumuishi za afya nchini.
Mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Makatibu wa Afya wa Mikoa, Wafamasia, Wataalamu wa Maabara, Waratibu wa VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu, Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za afya nchini.







