
Na Sixmund Begashe, Dodoma
PROGRAM ya SPACES ambayo inatekelezwa na Kampuni ya McKinsey & Company ya nchini Marekani imeonesha nia yake ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutoa msaada wa kiufundi, hasa kujenga uwezo wa Wataalam kwenye uhifadhi wa maliasili nchini.
Akizungumza katika wasilisho lake kwa uongozi wa Idara ya Wanyamapori, Jijini Dodoma leo Julai 21,2026, Mtaalam kutoka Kampuni ya McKensey & Company Bi. Gillian Pais, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inafanya kazi nzuri ya uhifadhi hivyo wameona ni vyema wakaunga mkono juhudi hizo.
Bi. Pais ameongeza kuwa, lengo kuu la wasilisho lake ni kutambulisha Program ya SPACES na kujadiliana namna gani Serikali kupitia Wizara hiyo inaweza kushiriki kwenye Program hiyo ili kuchechemua zaidi shughuli za uhifadhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Mkurugenzi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora ameipongeza Kampuni hiyo kwa nia yake hiyo na kuahidi kuwa ofisi yake itatoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha hatua zote za ushirikiano kwa kuwa moja ya malengo ya Wizara ni kushirikiana na wadau katika uhifadhi endelevu wa maliasili ikiwemo Sekta ya Wanyamapori.
Kikao hicho chenye sura ya kufungua zaidi ukurasa wa kuwajengea uwezo wataalam wa uhifadhi pamoja na kuandaa maandiko yanayovutia wahisani na wafadhili, kimehudhuriwa pia na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Bi. Kay Kagaruki na wataalam wa Idara hiyo.
