Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na Menejimenti na watumishi wa Makumbusho ya Taifa la
Tanzania katika Makao Makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo tar 20/7/2026
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akizungumza na Menejimenti na watumishi wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika Makao Makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo tar 20/7/2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi akiwa katika  onesho la kudumu la ndege ya kwanza ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere
leo tar 20/7/2026
Picha ya pamoja kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga pamoja na watendaji wa Makumbusho ya Taifa pamoja an wadau mbalimbali.
……………………

Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Julai 20, 2026 amekutana na
Menejimenti na watumishi wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika Makao Makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, kwa kikao cha kutathmini utekelezaji wa shughuli za mwaka wa fedha uliopita na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
 

Dkt. Abbasi, ambaye
amepokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, amesema Makumbusho ya Taifa ni taasisi muhimu yenye jukumu la kuhifadhi historia, utamaduni na urithi wa Taifa, huku akisisitiza kuwa mchango
wa sekta hiyo unapaswa kuonekana katika maendeleo ya nchi.

“Sekta hii ina
mchango wake kwa jamii, siasa na uchumi, na mchango huo unatakiwa uonekane. Misingi imara inatakiwa kuwekwa ili taasisi iweze kutimiza wajibu wake kwa ufanisi,” amesema Dkt. Abbasi.
 

Amesema ni muhimu
kuimarisha misingi ya taasisi kwa kuweka mikakati endelevu ya kuongeza mapato na kushirikisha wadau katika shughuli za kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Taifa.
 

Aidha, amekielekeza
Kitengo cha Masoko na Uhusiano kuandaa programu mbalimbali za masoko na utangazaji zitakazoongeza mwonekano wa Makumbusho ya Taifa, kuvutia wageni wengi zaidi na kuongeza mapato ya taasisi.
 

Dkt. Abbasi amesema
Serikali itaendelea kushirikiana na Makumbusho ya Taifa kwa kutoa ushirikiano na msaada unaohitajika ili kuboresha huduma, kuimarisha uhifadhi wa urithi wa Taifa na kuongeza mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga ametumia fursa hiyo kusema kuwa Makumbusho itaendelea kufanya tafiti,kuihifadhi na kuielimisha jamii kuhusu urithi wa utamaduni.

Baada ya kikao hicho,
Katibu Mkuu ametembelea onesho la kudumu la ndege ya kwanza ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo alielekeza kufanyika maboresho zaidi ya eneo hilo ili wageni wapate fursa bora ya kujifunza historia ya chombo hicho cha kipekee na nafasi yake katika historia ya Taifa hasa tunapoelekea katika mashindano ya AFCON 2027.