KARIBU NYUMBANI, NGORONGORO IMEWAFIKIA OMAN

 Mwandishi Wetu,

Mwambata wa ubalozi  wa Oman nchini Tanzania, Abdulrahman Salim Algaad akiwa na familia yake, ametembelea Hifadhi ya Ngorongoro  na kushuhudia maajabu ya utalii yaliyopo katika kivutio namba moja cha utalii barani afrika.

Akimpokea mwambata huyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko  Mariam  Kobelo ameeleza kuwa jitihada za mamlaka hiyo kuwafikia wadau mbalimbali zimeendelea kuzaa matunda ambapo watumishi kutoka balozi mbalimbali ndani na nje ya nchi wamendelea kutembelea hifadhi hiyo.

Akiwa ndani ya hifadhi hiyo, Abdulrahman Algaad na familia yake walipata fursa ya kushuhudia wanyamapori adimu wakiwa katika mazingira yao ya asili, wanyamapori wakubwa watano, misitu, maporomoko ya maji, urithi wa utamaduni na mambo kale, makumbusho ya urithi geopark na kueleza kuwa ndoto na hisia alizokuwa nazo zimekutana na uhalisia.

Mwambata huyo ameonyesha kuvutiwa na uzuri wa Hifadhi ya Ngorongoro na vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na kupongeza hatua za uhifadhi zinazofanyika na kuifanya Ngorongoro kuendelea kuheshimika kimataifa na kuwa eneo la urithi wa dunia lenye hadhi tatu za kimataifa.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia huduma za utalii na masoko, Mariam Kobelo amebainisha kuwa ziara za viongozi na maafisa wa kidiplomasia wanaotembelea Ngorongoro zinachangia kuitangaza Tanzania kimataifa, kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, kuongeza ushirikiano kupitia diplomasia ya uchumi.


Post a Comment

Previous Post Next Post