PUMA ENERGY TANZANIA YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 15 KWA SERIKALI


 Dar es Salaam. Kampuni ya Puma Energy Tanzania imekabidhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania gawio la shilingi bilioni 15, ikiwa ni nusu ya faida iliyopatikana, hatua inayotajwa kuwa ni gawio kubwa zaidi kutolewa katika historia ya kampuni hiyo.

Gawio hilo lililowasilishwa kwa Serikali linaonesha mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kupitia umiliki wa pamoja wa hisa ambapo Serikali inamiliki asilimia 50 ya hisa za Puma Energy Tanzania.

Hundi hiyo ilipokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Tanzania pamoja na viongozi wa kampuni hiyo.

Gawio hilo limeongezeka kwa asilimia 11 ikilinganishwa na shilingi bilioni 13.5 zilizotolewa mwaka 2025, jambo linaloonesha kuimarika kwa utendaji wa kifedha wa kampuni hiyo pamoja na uwekezaji wake wa kimkakati katika sekta ya nishati nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliipongeza Puma Energy Tanzania pamoja na kampuni nyingine zinazotekeleza wajibu wao kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya taifa kupitia ushirikiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy Tanzania, Balozi George Madafa, alisema gawio hilo ni matokeo ya uimara wa biashara ya kampuni pamoja na mkakati wake wa ukuaji wa muda mrefu.

“Makabidhiano ya gawio la leo yanaakisi utendaji mzuri wa Puma Energy Tanzania, uimara wake na dhamira ya kuendelea kuzalisha thamani endelevu kwa wanahisa wetu na taifa kwa ujumla,” alisema Balozi Madafa.

Alisema ongezeko la gawio hilo linatokana na uimara wa mfumo wa biashara wa kampuni, kujituma kwa wafanyakazi pamoja na imani ya wateja wanaoendelea kutumia huduma za kampuni hiyo.

Balozi Madafa aliongeza kuwa kupitia umiliki wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Puma Energy, mafanikio ya kampuni yanaendelea kunufaisha Watanzania kupitia gawio kwa wanahisa, ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali, uwekezaji pamoja na uanzishaji wa ajira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema kampuni itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati na suluhisho bunifu zitakazosaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Alisema katika miaka ya hivi karibuni kampuni imewekeza katika kupanua mtandao wa vituo vya huduma, kuimarisha usambazaji wa mafuta ya ndege, kukuza biashara ya gesi ya LPG pamoja na kuanzisha matumizi ya nishati safi kama Gesi Asilia Iliyobanwa (CNG).

“Uwekezaji huu unaweka msingi imara wa ukuaji wa baadaye, unaunga mkono ajenda ya maendeleo ya viwanda na mabadiliko ya matumizi ya nishati, huku tukiendelea kutoa huduma za nishati za kuaminika,” alisema Fatma.

Alisema ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali, huku ikitambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa rekodi yake nzuri ya ulipaji kodi.

Puma Energy Tanzania ina zaidi ya vituo 100 vya huduma za mafuta, kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta pamoja na maghala mbalimbali nchini.

Kampuni hiyo pia inasambaza mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege vinane nchini, ikiwemo viwanja vyote vya kimataifa, huku ikiendelea kuwekeza katika nishati safi kupitia Kituo Kikuu cha CNG (CNG Mother Station) pamoja na vituo vya CNG vilivyopo Dar es Salaam na Morogoro.

Aidha, kampuni inaendelea kupanua huduma za nishati safi za kupikia kupitia Puma Gas, huku biashara ya vilainishi na maduka ya Shop Express yakiendelea kutoa bidhaa na huduma mbalimbali kwa wateja

Post a Comment

Previous Post Next Post