DAR ES SALAAM, Julai 30, 2026 – Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametangaza kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yatafanyika kuanzia Agosti 15 hadi 20 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga, yakilenga kuonyesha mchango wa elimu, ujuzi na ubunifu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Profesa Mkenda amesema maadhimisho hayo yatawakutanisha wizara mbalimbali, taasisi za elimu ya juu, taasisi za utafiti, vyuo vya ufundi, vyuo vya ualimu, shule, wabunifu, watafiti, kampuni za teknolojia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili na kuonyesha mafanikio ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”, ikiwa inalenga kuhamasisha matumizi ya maarifa na teknolojia katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Profesa Mkenda amesema maadhimisho hayo yatajumuisha maonyesho ya teknolojia, bidhaa na bunifu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), mashindano ya ujuzi kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi, makongamano ya kitaaluma, warsha pamoja na utoaji wa huduma kuhusu hakimiliki na ulinzi wa bunifu.
Amesisitiza kuwa kupitia mashindano ya MAKISATU, Serikali imefanikiwa kuibua bunifu nyingi ambazo tayari zimeingia sokoni na kuanza kuwanufaisha wabunifu wake. Miongoni mwa bunifu hizo ni mashine ya kukamua mafuta ya parachichi (Avomero), mabegi ya shule yenye mfumo wa sola, vifaa vya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu, teknolojia za kuchakata vyakula vya mifugo pamoja na mita janja za maji.
“Wapo wanaodhani bunifu zinaishia kwenye maonyesho pekee, lakini ukweli ni kwamba zipo nyingi ambazo tayari zimeingia sokoni na wabunifu wake wanafanya biashara. Serikali inaendelea kuwawezesha wabunifu kuhakikisha teknolojia zao zinawanufaisha wananchi na uchumi wa taifa,” amesema Profesa Mkenda.
Aidha amesema Serikali inaendelea kusimamia takribani bunifu 70 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za maendeleo, huku ikiimarisha mazingira ya kuzifikisha sokoni kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali pamoja na sekta binafsi.
Profesa Mkenda amesema Wizara imeanzisha Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika halmashauri mbalimbali nchini ili kurahisisha utambuzi na usaidizi wa wabunifu. Amesema hadi sasa halmashauri 90 tayari zimeanzisha madawati hayo na lengo ni kuyafikisha katika halmashauri zote nchini.
Pia amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeweka utaratibu wa kuwawezesha wabunifu kupata mitaji ya kuendeleza biashara zinazotokana na ubunifu wao, huku ikiendelea kushirikiana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kutafuta masoko, utaalamu na fursa za uwekezaji katika sekta ya sayansi na teknolojia.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazowakabili baadhi ya wabunifu, Profesa Mkenda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi husika kuhakikisha bunifu zinazohitaji uthibitisho wa kitaalamu zinakamilisha taratibu zote kwa wakati bila kuathiri viwango vya usalama, hususan kwa bidhaa zinazohusu afya.
Ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, watafiti, wabunifu, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 ili kujionea teknolojia na bunifu zinazotengenezwa na Watanzania pamoja na fursa zinazotokana nazo katika kukuza uchumi wa taifa.

