TANZANIA NA UJERUMANI ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA MAJI


 Mwandishi Wetu,

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amefanya mazungumzo na Kaimu Mkuu wa Idara ya Miradi ya Maendeleo katika Ubalozi wa Ujerumani nchini. Bi. Marlene Landes, jijini Dar es Salaam.

Lengo la mazungumzo hayo ni kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani katika kuendeleza Sekta ya Maji.  

Katibu Mkuu, Mhandisi Mwajuma Waziri amesisitiza kuwa ushirikiano huo ujikite zaidi katika maeneo ya kimkakati ili kuongeza tija katika sekta. Akitaja umuhimu wa kujenga uwezo wa wataalamu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia, kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya SCADA katika uendeshaji na ufuatiliaji wa miundombinu. 

Aidha, ameongeza kuwa kuna haja ya kuendeleza matumizi ya Green Bonds kama chanzo mbadala cha fedha za uwekezaji, pamoja na kuhimiza matumizi ya vifaa vyenye ufanisi mkubwa wa nishati ya jua.

Mhandisi Mwajuma amebainisha  kuwa Sekta ya Maji bado inahitaji vyanzo mbadala vya fedha na ushirikiano wa kiufundi ili kuharakisha utekelezaji na ukamilishaji wa miradi nchini. 

Pia, ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia KfW na GIZ kwa mchango wake mkubwa wa muda mrefu katika kufanikisha malengo ya sekta na kuboresha huduma za maji kwa wananchi.

Kwa upande wake, Bi. Landes alithibitisha dhamira ya Serikali ya Ujerumani kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika Sekt ya Maji, akibainisha maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.  

Kikao hiki muhimu ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Serikali za kuchochea maendeleo ya Sekta ya Maji nchini kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo.


Post a Comment

Previous Post Next Post