
Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga fedha za kununua bidhaa za afya ikiwemo afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na uzazi wa mpango na kugharamia mafunzo kwa watumishi wa afya ili kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kutolewa kwa ufanisi baada ya kumalizika kwa mradi wa afya ya uzazi na uzazi wa mpango uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka tisa nchini.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Juni 18, 2026 wakati wa kongamano la kujifunza kuhusu upanuzi wa programu ya uzazi wa mpango na kufunga mradi huo uliofanyika katika ukumbi wa Mabeyo mkoani Dodoma.
“Niwahakikishie Watanzania, kuisha kwa mradi huu haimaanishi kwamba huduma zimekwisha, huduma zitaendelea kama kawaida kwa sababu kwa kipindi cha miaka Tisa, Serikali imetenga rasilimali fedha, kujenga uwezo wa watumishi na mifumo na sasa tunatoa huduma zote za afya ya uzazi na mtoto kwa mfumo wa kawaida kupitia vituo vya umma na watu binafsi,” amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema mradi huo uliotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Elimu, washirika wa maendeleo na mamlaka za serikali za mitaa umechangia kuimarika kwa huduma za afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa wananchi.
“Moja ya mafanikio makubwa ya mradi huu ni kujengewa uwezo kwa wataalamu wa afya ili kutoa huduma bora za afya ya uzazi kwa makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu sambamba na kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi wa bidhaa za afya ya uzazi nchini,” amesema Dkt. Magembe
Kwa upande wa elimu, Dkt. Magembe amesema kupitia ushirikiano na Wizara ya Elimu, walimu walijengewa uwezo wa kutoa elimu sahihi ya afya ya uzazi kwa vijana na wanafunzi ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi na kupunguza mimba za utotoni pamoja na changamoto nyingine zinazowakabili vijana.
Pia, Dkt. Magembe amesema mradi huo umesaidia makundi maalum hasa kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa na wao wanahitaji kuelewa na kujikinga na watu wenye nia ovu kwao na waweze kupata huduma hizo kwa kuzingatia mahitaji yao.
