Mwandishi Wetu,
Wananchi wa mitaa mbalimbali eneo la Kimara Stop over, Kata ya Kimara Wilaya ya Ubungo wameanza kupata huduma ya majisafi baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kufanya maboresho ya miundombinu.
Baadhi ya wananchi walioikosa huduma hiyo kwa kipindi kirefu wameipongeza DAWASA kwa jitihada za kuwarejeshea majisafi.
"Tumekosa huduma ya maji kwa kipindi kama cha mwezi mmoja, lakini toka jana usiku tumeendela kupata huduma ya maji hadi sasa, tunawashukuru DAWASA kwa kuchukua hatua za lazima ili kuhakikisha tunapataa huduma hii muhimu" amesema Ndugu Ashura Ally.
Ashura amesema kwa kipindi cha nyuma wamekua wakinunua maji kwa bei juu jambo ambalo halikuwa rafiki katika biashara zao.
"Tunaona mafundi wa DAWASA wakiendelea na matengenezo kuhakikisha nyumba chache ambazo hawajapata huduma ya maji yanawafikia pia, tunaomba baada ya maboresho haya huduma hii iwe endelevu" amesema Ndugu Ashura.
Akizungumzia Maboresho waliyofanya, Mhandisi Gabriel Shija amesema kwasasa wameelekeza maji eneo la Kimara Stop over na timu ya mafundi inaendelea kufuatiliaa kwa ukaribu kuhakikisha huduma inawafikiwa wananchi wote.
"Pamoja na mafanikio haya kuwafikishia huduma ya maji wananchi wa Stop over, bado kuna baadhi ya wananchi walikuwa hawapati maji.
“Tunaendelea na zoezi la kuunga bomba la inchi mbili kutoka eneo la kwa Babu mboga kuja Stop over mtaa wa Nogeza ili kuongeza wingi wa maji na leo hii hii wananchi hawa wote watapata huduma ya maji," amesema Mhandisi Shija.
Kukamilika kwa maboresho haya kutaboresha huduma ya maji katika maeneo ya Mazingira, Michungwani, Nogeza, Manzese na baadhi ya maeneo ya Kimara B huku maeneo mbalimbali kama vile Suka, Temboni, Kibanda cha Mkaa yakiendelea kupata huduma ya maji.

