Endelezeni elimu ya afya ya udongo kwa wakulima: Mkomi

Mwandishi Wetu,

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma S. Mkomi, ameishauri Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuendeleza juhudi za  kuwashauri wakulima kupima afya ya udongo ili waweze kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na mazao wanayolima na hivyo kuongeza tija kwenye kilimo chao.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Juni, 2026 alipopita kwenye banda la Mamlaka ili kuwashukuru kwa kushiriki na kuwahudumia wananchi   katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026.

Aidha, amewasihi kuendelea kujipanga na kushiriki kikamilifu katika maonesho kama hayo yatakayofanyika mwaka 2027.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, yalianza tarehe 16 Juni 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa kesho, tarehe 23 Juni 2026.

Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu huyo, Afisa Tehama wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Salehe Kejo amesema Mamlaka ina jukumu kubwa la kuhakikisha mkulima anapata mbolea Bora na kwa bei himilivu kwa kilimo endelevu na kulihakikishia taifa usalama wa chakula.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post