Mwandishi Wetu,Dodoma
Tume ya Madini imewataka wamiliki na waombaji wote wa leseni za utafiti na uchimbaji wa madini nchini kuhakiki taarifa zao za leseni na maombi kabla ya Juni 25, 2026, ili kuboresha mfumo wa usimamizi na utoaji wa leseni za madini nchini.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Tume, zoezi hilo linahusisha wamiliki wa leseni za utafiti, uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa wa madini pamoja na waombaji wa leseni mbalimbali za madini.
Taarifa zinazotakiwa kuhakikiwa ni pamoja na anuani zinazojumuisha sanduku la posta, barua pepe, namba za simu pamoja na jina na namba za simu za msimamizi wa mfumo wa portal.
Vilevile, wahusika wanatakiwa kuwasilisha namba ya mlipa kodi (TIN), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au pasi ya kusafiria, pamoja na nyaraka za kampuni ikiwemo Brela Search au MEMART endapo kutakuwa na mabadiliko ya wakurugenzi.
Aidha, Tume imeeleza kuwa nguvu ya kisheria (Power of Attorney) ya msimamizi wa portal nayo ni miongoni mwa nyaraka muhimu zinazopaswa kuwasilishwa katika zoezi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhakiki unaweza kufanyika kupitia Mfumo wa Huduma za Leseni za Madini kwa njia ya mtandao (OMCTP) kupitia tovuti ya portal.madini.go.tz au kwa kuwasilisha taarifa hizo katika ofisi za Tume ya Madini.
Leseni za utafiti pamoja na uchimbaji wa kati na mkubwa zitahudumiwa Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, huku leseni za uchimbaji mdogo zikihudumiwa katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zilizopo karibu na maeneo ya shughuli za wachimbaji.
Tume ya Madini imeonya kuwa kushindwa kuhakiki taarifa hizo kutasababisha kuondolewa kwa maombi au leseni zenye upungufu katika mfumo wa usimamizi na utoaji wa leseni za madini.
Akizungumza kupitia tangazo hilo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Ramadhani M. Lwamo, amewasisitiza wadau wa sekta ya madini kutoa ushirikiano katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.

