WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI STAMICO, WAANZA ZIARA YA KUTEMBELEA MIRADI YA SHIRIKA KANDA YA ZIWA


 Na Nasra Ismail



📍Lwamgasa, Geita

Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo 11 Mei, 2026 imefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya Shirika hilo iliyoko kanda ya Ziwa. Lengo la ziara hiyo ni kujionea utekelezaji na kuhakikisha miradi inatekelezwa kama ilivyopangwa na kukidhi malengo yaliyowekwa na Shirika.

Wajumbe wa bodi hiyo wametembelea kwanza kituo bora cha mfano kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu uliopo katika Kata ya Lwamgasa, Wilaya ya Geita. Mradi huo hutumika kama darasa la kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Akizungumza moja ya wajumbe hao Bw. Leonard Chacha, amesema mgodi wa Lwamgasa ni mgodi wa mfano nchini. Amesisitiza kuwa kupitia mgodi huo, wachimbaji wanafundishwa namna bora ya kuchimba kisasa ili kuongeza tija na kuhakikisha usalama wao wakati wa kazi na utunzaji wa mazingira.

Chacha aliongeza kuwa pamoja na mafunzo ya uchimbaji, wachimbaji hao pia huwezeshwa kutumia mashine za kisasa katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu. Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwaondoa wachimbaji wadogo kwenye teknolojia duni inayowapotezea madini mengi na kuharibu mazingira.

Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, wajumbe wa bodi walitembelea Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef ambao STAMICO inauendesha kwa ubia na kampuni ya TRX Gold Corporation. Wajumbe hao walipata wasaa wa kupata taarifa ya mradi na kukagua shughuli mbalimbali za uzalishaji kuanzia uchimbaji hadi uchenjuaji.

Aidha, Wajumbe wa bodi wameridhishwa na hali ya utunzaji wa mazingira katika mgodi wa Buckreef. Wamesema uongozi wa mgodi umeweka mikakati mizuri ya kuhakikisha shughuli za uchimbaji hazileti madhara kwa mazingira yanayozunguka eneo la mradi.

Wilson Mutagwaba, Mjumbe wa Bodi ya STAMICO, amekiri kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika mgodi wa Buckreef. Amesema pamoja na utunzaji wa mazingira, suala la usalama mahali pa kazi limepewa kipaumbele kikubwa na wafanyakazi wote wanafuata taratibu za usalama.

Bodi ya Wakurugenzi imeahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika kufanikisha shughuli za Shirika na kuendelea kufanya ziara za mara kwa mara katika miradi yote ya STAMICO nchini. Lengo ni kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na tija kwa Taifa, inalipa kodi stahiki na inawanufaisha wananchi wanaozunguka maeneo ya miradi hiyo.











Post a Comment

Previous Post Next Post