NA MWANDISHI WETU
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo Mei 11, 2026, imetoa mafunzo kwa Majaji wa Mahakama Kuu na Manaibu Wasajili wa Divisheni ya Biashara kuhusu haki za miliki ubunifu, kwa lengo la kuimarisha usimamizi na ulinzi wa haki hizo nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Kiongozi, Jaji Imani Aboud amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uelewa na kubadilishana uzoefu katika eneo la miliki ubunifu.
“Maendeleo ya nchi yoyote yanategemea ubunifu. Hata hivyo, wamiliki wa ubunifu huo wamekuwa wakikumbana na changamoto za kisheria zinazofikishwa mahakamani. Ni muhimu kwa sisi tunaosikiliza na kutafsiri sheria kuelewa kwa kina masuala haya ili kuhakikisha haki zinatendeka ipasavyo,” amesema Mhe. Jaji Aboud.
Ameongeza kuwa maamuzi ya mahakama yana athari pana, kwani hutumika kama rejea hata katika nchi nyingine, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na uelewa wa kina kuhusu haki za miliki ubunifu.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, Dkt. Cleoface Morris, amesema kuwa mashauri mengi yanayofunguliwa mahakamani yanahitaji tafsiri sahihi ya sheria ili kuimarisha usimamizi wa haki za miliki ubunifu.
“Mafunzo haya yatatusaidia kuwa na uwiano katika utoaji wa maamuzi ndani ya Mahakama Kuu, hasa kwa kuzingatia kuwa mashauri mengi yanafanana kimuktadha,” amesema Dkt. Morris.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za taasisi hiyo kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, hususan katika eneo la miliki ubunifu ambalo bado linahitaji uelewa mpana zaidi nchini.
Ameeleza kuwa maamuzi ya majaji yana mchango mkubwa katika kulinda maslahi ya taifa katika sekta ya miliki ubunifu, na kwamba tayari zipo hukumu kadhaa ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya BRELA.
“Tumeleta wataalam wa miliki ubunifu ili kujenga uelewa wa pamoja. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo kila ubunifu unalindwa kisheria, kwa kuwa ni chanzo muhimu cha kipato kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Nyaisa.
BRELA imekua ikitoa Mafunzo ya Miliki Ubunifu kwa Majaji na Wadau mbalimbali wa Sheria nchini ili kuboresha na kurahisisha Utoaji wa Huduma na kujenga uelewa mpana wa Miliki Ubunifu kwa jamii.


