NA MAGENDELA MRISHO, KARATU
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha Englibert Qorro, ameiomba Serikali kuisapoti Taasisi ya Iles De Paix In Tanzania (IDP) yenye makao yake jijini Arusha, ili iendelee kuwekeza kwenye kilimo Ikolojia.
Pia ameweka wazi kwamba Karatu kwa sasa wanaanza kupunguza ufugaji na kuingia katika nyanja ya kilimo hivyo ni vyema wananchi wa wilaya hiyo wakaendelea kupatiwa elimu ya kilimo ikolojia ili iweze kusambaa katika maeneo mengi.
Kiongozi huyo amezunguza hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari za Kilimo Ikolojia waliofika wilayani humo, Machi 24 mwaka huu kujionea mafanikio ya wakulima waliopatiwa elimu ya kilimo hicho namna wanavyotunza mbegu asili, wanavyotengeza mbolea samadi na viwatilifu visivyo na kemilikali na wanavyonufaika kupitia mazao wanayolima.
“Kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu na mtalaam wa mazingira, nimefurahi kuwaona hapa pamoja na wataalamu kutoka taasisi ya IDP ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kuwapata elimu ya Kilimo Ikolojia nawaomba msichoke, sambazeni elimu hii karatu nzima.
Karatu ni eneo muhimu na ufugaji umepungua na sasa tumeingia kwenye kilimo, kama mtaalam ninaiomba Serikali iwepe sapoti kuwekeza kwenye kilimo na kuwawezesha wananchi wa karatu kupiga hatua zaidi kupitia Kilimo Ikolojia, amesema.
Baadhi ya wakulima wilayani humo walipatiwa mafunzo ya namna ya kujikita kwenye misingi ya mifumo endelevu ya chakula kwa kutumia Kilimo Ikolojia ambacho kimekuwa na matokeo mazuri kuanzia kwa wakulima hadi walaji.
Kwa maana wakulima wamekuwa hawapati madhara wakati wote wa kulima hadi kuvuna kutokana pembejeo wanazotumia shambani ni za asili hali inayofanya hata zao linapomfikia mlaji kuwa salama kwa afya yake.
