
Watoa Msaada kwa Makundi Maalum
📍Hombolo, Dodoma.
Watumishi wa Wizara ya Madini leo Machi 31, 2026, wamepeleka tabasamu kwa jamii yenye uhitaji maalumu kwa kwa watoto yatima na wazee wasiojiweza wa Kituo cha Watoto cha Huruma kilichopo Hombolo, kinachoendeshwa na Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia.
Akikabidhi misaada hiyo Kwa niaba ya Watumishi wa Wizara ya Madini Makao Makuu, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala kutoka Wizara ya Madini, Bi. Beatrice Matemu, ambaye alikua kiongozi wa msafara amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya watumishi wa wizara hiyo kutoa kwa jamii sehemu ya kile wanachopata, hususan kwa makundi yenye uhitaji maalum kuelekea Sikukuu ya Pasaka.
Kwa upande wake, msimamizi wa kituo hicho, Sista M. Judy Claris, amesema kwa sasa kituo kinahudumia watoto 29 wenye umri wa kati ya miezi miwili hadi miaka minne na nusu, wanawake 27 pamoja na wanaume 25 wenye changamoto mbalimbali zinazohitaji uangalizi wa karibu na huduma endelevu.
Ameeleza kuwa pamoja na kulea na kuhudumia makundi hayo katika kituo hicho, wao pia hutoa misaada kwa jamii inayowazunguka, ambapo kila siku ya Jumanne hugawa vyakula kama mboga, unga na sukari, pamoja na kupika chakula kwa wahitaji wanaofika kituoni hapo.
Sista Judy ametoa wito kwa wadau na watu wengine kujitokeza kusaidia kituo hicho ili kiweze kuendelea kutoa huduma, akibainisha kuwa kwa sasa wanategemea zaidi shughuli ndogo za kilimo cha mbogamboga, njugu na maharage, pamoja na ufugaji wa ng’ombe kama chanzo cha kujikimu.
Katika ziara hiyo, watumishi wa Wizara ya Madini walikabidhi msaada uliojumuisha mahitaji muhimu ya kila siku kama mchele, unga, sabuni, unga wa lishe, taulo za kike, mafuta ya kupikia, chumvi, juisi na biskuti kwa ajili ya watoto.
Aidha, imeelezwa kuwa makundi hayo yanahitaji kwa kiasi kikubwa mahitaji ya msingi ya maisha ya binadamu ikiwemo chakula, mavazi, malazi pamoja na huduma za afya na dawa wanapougua.
Ziara hiyo imeacha alama ya faraja kwa wahitaji wa kituo hicho, huku ikisisitiza umuhimu wa mshikamano na upendo katika kujenga jamii inayojali na kuthamini utu wa kila mmoja.
