UKANDA WA NYASA MBIONI KUFAIDI UMEME REA

 

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) inakamilisha mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vya ukanda wa Nyasa, baadhi vikiwa ndani ya Ziwa Nyasa. Vitongoji hivyo viko Ludewa, mkoani Njombe, na vingine Kyela, mkoani Mbeya, ambavyo ndani ya mwezi ujao vitafaidika na umeme wa uhakika.

Msimamizi wa Miradi wa REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Danstan Kalugira, amesema vitongoji sita vitakavyofaidika ni Kitewele na Kimata (Ludewa) na Kiguru, Chanjale, Lumbuta na Nkanda (Kyela). Mradi ulianza Julai 13 mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Aprili 13 mwaka huu.

Kalugira alisema mradi unatekelezwa na mkandarasi SUMA JKT kwa gharama ya Sh. bilioni 3.1, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kutandaza waya za umeme. Umeme unasafirishwa katika kilovoti 33 kutoka Kijiji cha Madunda, Kata ya Mawengi, hadi vitongoji husika.

Msimamizi wa Mradi wa SUMA JKT, Yassin Selemani, amesema changamoto kubwa ni miundombinu ya barabara, mvua na milima, jambo linalolazimisha kusimika nguzo moja kwa siku. Hadi sasa nguzo 105 zimeshafungwa na sasa wanangojea kutandazwa kwa nyaya.

Kalugira pia alisema vijiji vyote 381 vya Mkoa wa Njombe vina umeme, huku kati ya vitongoji 1,833 vya mkoa huo, 1,249 vimeshafikiwa na umeme na 584 bado vimesalia. REA Nyanda za Juu Kusini inahudumia mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Ruvuma.

Post a Comment

Previous Post Next Post