
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika Machi 12, 2026, jijini Dodoma.
………..
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema mpango wa utoaji wa chakula mashuleni una mchango mkubwa katika kuboresha mahudhurio, afya na ufaulu wa wanafunzi nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni pamoja na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika Machi 12, 2026 jijini Dodoma.
Amesema kuwa mpango wa chakula mashuleni umeendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika kusaidia wanafunzi kupata lishe bora pamoja na kuongeza uwezo wao wa kuzingatia masomo wakiwa darasani.
Aidha amebainisha kuwa watoto hutumia muda mwingi wakiwa shuleni, hivyo upatikanaji wa chakula bora, maji safi na mazingira salama ya usafi ni mambo muhimu katika kuhakikisha wanakuwa na afya njema na mazingira bora ya kujifunzia.
Pia ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha miundombinu na mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji nchini.
Amesema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Chakula Bora, Maji Safi Shuleni: Ni Wajibu wa Pamoja,” ambayo inalenga kuhimiza ushirikiano kati ya serikali, wadau wa maendeleo na jamii katika kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma muhimu shuleni ikiwemo chakula, maji safi na huduma za afya.
Aidha amesema kuwa utekelezaji wa mpango wa chakula na lishe shuleni unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, maji na maendeleo ya jamii pamoja na mashirika ya maendeleo na yasiyo ya kiserikali.
Pia ameongeza kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI inapaswa kuendelea kufuatilia vyakula vinavyouzwa katika maeneo ya shule ili kuhakikisha vinakuwa salama kwa matumizi ya wanafunzi na vinaendana na miongozo ya Shirika la Afya Duniani kuhusu afya ya umma.
Amesema kuwa wadau wa elimu wanapaswa kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu muhimu shuleni ikiwemo ujenzi wa stoo za chakula, mabwalo ya kulia chakula, majiko ya kupikia pamoja na matumizi ya nishati safi na uwepo wa vituo vya kunawia mikono.
Aidha amebainisha kuwa ushirikiano kati ya serikali, wadau na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora na mazingira mazuri ya kujifunzia, hali itakayosaidia kufikia lengo la kutoa elimu bora na jumuishi nchini.
Katika maadhimisho hayo, serikali pia imewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UNICEF, World Food Programme (WFP), GAIN Tanzania na Sanku kwa mchango wao katika kuunga mkono juhudi za kuboresha lishe na huduma ya chakula mashuleni.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo, Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), Bi. Christin Mendezi, amesema kuwa wanaipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za kuimarisha na kupanua mpango wa utoaji wa chakula mashuleni ambao umeonesha matokeo chanya katika kuboresha afya, mahudhurio na ufaulu wa wanafunzi.
Aidha amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, mpango wa chakula mashuleni umechangia kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa asilimia tisa na mahudhurio kwa asilimia kumi, huku pia ukisaidia kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa asilimia ishirini miongoni mwa watoto wa umri wa kwenda shule.
Pia ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kuonesha uongozi mzuri katika utekelezaji wa mpango wa chakula mashuleni kupitia miongozo ya kitaifa ya lishe shuleni, ushiriki wa jamii pamoja na kuunganisha uzalishaji wa chakula kutoka kwa wakulima wa ndani.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chakula na Lishe kutoka Mkoa wa Njombe, Fadhili Msiru, amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa chakula mashuleni katika mkoa huo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya serikali, wazazi na jamii kwa ujumla