
JOHANESBURG, AFRIKA KUSINI: Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Johannesburg na uongozi wa chuo hicho kukutana na wanafunzi wa Kitanzania 16 wanaosomea kozi mbalimbali chuoni hapo chini ya mpango wa Samia Scholarship Extended (SSE).
Kupitia udhamini huo, Tanzania ilipeleka wanafunzi hao nchini Afrika Kusini kusomea shahada za Kwanza za masomo ya kompyuta; akili unde (AI); sayansi ya takwimu na tahsusi nyingine za sayansi na teknolojia.
Madhumuni ya Naibu Waziri kutembelea chuo hicho Jumatano (Machi 25, 2026) mashuhuri Afrika yalikuwa ni kukutana na uongozi mkuu wa taasisi hiyo ya elimu ya juu ili kufungua fursa zaidi za ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya Tanzania pamoja na Afrika Kusini.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, viongozi na waratibu wa Samia Scholarship Extended (SSE) pamoja na maafisa waandamizi kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Mara baada ya kuwasili chuoni hapo, ujumbe ulioongozwa na Wanu ulipokelewa na Profesa Refilwe Phaswana-Mafuya, makamu mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia utafiti na uvumbuzi, pamoja na viongozi wengine wa juu wa Chuo Kikuu cha Johannesburg.
Ziara hiyo imewezesha kuimarisha uhusiano wa kielimu na kisayansi kati ya Tanzania na Afrika Kusini na kufungua majadiliano ya kuanzisha Kozi za Ufundishaji wa Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu hicho.
Jumanne, wiki hii, Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuongeza juhudi za kutekeleza Hati ya Makubaliano (MoU) ya mwaka 2022 kuhusu ushirikiano katika elimu ya msingi, kwa lengo la kukuza ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za Afrika Kusini.
Mnamo Agosti 2022, nchi hizo mbili wanachama wa SADC zilitia saini makubaliano hayo kama sehemu ya juhudi za kukuza lugha hiyo na ushirikiano wa kikanda.
Katika mkutano huo, Wanu alieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha elimu, sayansi na teknolojia.
Kuhusu Kifungu cha 9 cha MoU, viongozi hao wawili walisisitiza umuhimu wa utekelezaji madhubuti wa kifungu hicho ili kukuza Kiswahili kimataifa na kuimarisha mshikamano wa kikanda kupitia elimu.
Kupitia mazungumzo hayo, Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu, ikiwemo kupanua programu za ubadilishanaji wa walimu na wataalamu katika elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu, pamoja na kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi.

Maeneo mengine ni pamoja na kuimarisha programu za tafiti, kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi na vyuo vya elimu ya juu, pamoja na kuongeza fursa za ufadhili wa masomo.
Serikali ya Tanzania pia imeeleza dhamira yake ya kupanua fursa kwa vijana wa Kitanzania wanaonufaika na programu mbalimbali za ufadhili wa masomo, ikiwemo Samia Scholarship.
Pande zote mbili pia zimesisitiza umuhimu wa kuendeleza programu za pamoja zitakazochochea ubunifu, uhamishaji wa teknolojia na kuboresha ubora wa elimu katika nchi zote mbili.