Mwandishi Wetu,
Wakulima wa vijiji vya Kibedya na Rubeho katika Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro wamehimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya pembejeo na kupima afya ya udongo ili kuongeza tija, kulinda mazingira na kuinua kipato kupitia kilimo cha kisasa.
Akizungumza na wakulima wa vijiji hivyo Februari 17, 2026 Afisa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Alphonce Mwiru amesema Serikali inaendelea na zoezi la upimaji udongo nchi nzima ili kubaini mahitaji halisi ya virutubisho kwenye mashamba.
Amesema hatua hiyo itawawezesha wakulima kufanya matumizi sahihi ya mbolea kulingana na aina ya udongo.
Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), John Wambura , amesisitiza kuwa mafanikio ya matumizi ya pembejeo yanategemea upimaji wa afya ya udongo na kuwasihi wakulima kupima mashamba yao kabla ya kutumia mbolea.
Naye Afisa Masoko kutoka TFC, Is-haq Ibrahim Mwalimu, amewataka wakulima kujiandikisha kwenye mfumo wa kidijitali wa ruzuku ili kupata mbolea kwa bei himilivu na kwa wakati, akieleza kuwa mfumo huo unaongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima Dani Mashasha na Twaha Ramadhani wamesema elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo imeongeza uelewa na matumaini ya mavuno bora, wakisisitiza umuhimu wa kuachana na kilimo cha mazoea na kuhamia kwenye kilimo cha kisasa chenye tija.
Aidha, Afisa Kilimo wa Kijiji cha Kibedya, Rahim Hamis, amesema wameanzisha mashamba darasa kwa lengo la kuwafundisha wakulima kwa vitendo mbinu bora za kilimo, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao katika Wilaya ya Gairo.





