Vijana watakiwa kuona fursa kwenye Kilimo

Mwandishi Wetu,

Vijana wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara watakiwa kuchangamkia fursa za kilimo cha kibiashara kwa kuzingatia matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo ili kuongeza tija na kipato. 

Wito huo umetolewa tarehe 24 Februari 2026 katika mwendelezo wa Kampeni ya Mali Shambani inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

Akizungumza wakati akiwakaribisha mkoani humo ,watalaam kutoka Wizara ya Kilimo , Taasisi zake pamoja na kampuni za mbalimbali za mbolea na mbegu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Manyara anayesimamia Sekta ya Uchumi na Uzalishaji, Faraja Ngerageza, alisema taifa linategemea kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi na chanzo cha kulifanya taifa kuwa ghala la chakula Afrika. 

Alisema kuwa hakuna kilimo chenye tija bila matumizi sahihi ya pembejeo, akiwahimiza vijana kutumia fursa zilizopo ikiwemo ruzuku ya mbolea na huduma za upimaji afya ya udongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Almishi Hazali, alisema zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya Halmashauri yanatokana na kilimo, akiongeza kuwa mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo ruzuku ya pembejeo,  na elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo inatoa nafasi kwa vijana kuingia kwenye kilimo cha biashara.

 “Hata mimi ni mkulima wa kibiashara; kilimo kina faida na kinahamasisha vijana kujiajiri,” alisisitiza.

Naye mkulima wa mahindi katika kijiji cha Masakta, Salome Msuya,Aliwahimiza vijana kujiingiza katika kilimo kwa kuwa sasa ni biashara yenye tija na mafanikio yanayoonekana.

Kilimo kinaendelea kuwa mhimili muhimu wa kuinua uchumi wa vijana na jamii kwa ujumla, hasa pale kinapofanywa kwa kuzingatia kanuni bora na matumizi sahihi ya pembejeo.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post