Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesisitiza umuhimu wa wakulima kujisajili katika mfumo wa kidijitali ili kuwezesha upatikanaji wa pembejeo hususan kupitia mpango wa ruzuku wa Serikali unaolenga kuongeza tija ya uzalishaji wa mavuno.
Akizungumza tarehe 23 Februari 2026 katika vijiji vya Kwamsisi na Kwasunga, wilayani Handeni mkoani Tanga, Afisa Udhibiti ubora kutoka TFRA Peter Mwanguku amesema usajili wa kidigitali wa mfumo wa pembejeo unasaidia kubaini mahitaji halisi ya pembejeo kwa kila eneo nchini.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Alphonce Mwiru amesema mfumo wa kidijitali umeongeza uwazi na ufanisi kwa kuwawezesha maafisa kilimo na wasimamizi wa pembejeo kufuatilia takwimu za wakulima, aina ya mazao wanayolima na mahitaji yao kwa misimu husika.
Naye mkulima Athumani Ibrahim Hassan kutoka kijiji cha Kwasunga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo akisema hatua hiyo itawawezesha wakulima kupata mavuno mengi na kuongeza kipato cha familia zao.
TFRA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Halmashauri imeendelea kutoa elimu na kuhamasisha wakulima kujisajili mapema ili kuhakikisha wananufaika kikamilifu na mpango wa ruzuku.









