
UPATIKANAJI wa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi 23.2 mwaka 2025, ongezeko la zaidi ya mara tatu ndani ya miaka minne. Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi, amesema mafanikio haya yanaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na nafuu, ikichangia kulinda afya, mazingira na kukuza uchumi.
Amesema Tanzania imeendelea kupanua matumizi ya nishati safi kupitia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Kwanza wa Afrika wa Nishati Safi ya Kupikia ambapo nchi ilihamasisha ahadi ya dola bilioni 2.2 kuendeleza sekta hiyo barani Afrika.
Waziri Ndejembi pia amebainisha kuwa Mei 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034 unaolenga kuratibu sera, mifumo ya kifedha na ushiriki wa sekta binafsi ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi. SOMA.

Kwa mwaka huu, Serikali inatarajia kusambaza majiko banifu 200,000 na mitungi 450,000 ya LPG kwa ruzuku, pamoja na kuanza majaribio ya kulipia vifaa vya kupikia kwa umeme kupitia bili za TANESCO. Aidha matumizi ya kuni na mkaa yamepigwa marufuku katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ikiwa ni pamoja na shule na vituo vya afya.
Waziri Ndejembi amesisitiza kwamba nishati safi ya kupikia ni sekta yenye fursa za ajira katika uzalishaji, usambazaji na matengenezo ya vifaa, na Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na kimataifa kuhakikisha malengo ya upatikanaji wa nishati safi yanafikiwa kwa ufanisi na endelevu.