VIJANA WATAKIWA KUOMBA MIKOPO YA UBUNIFU KUPITIA COSTECH

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Amier akizungumza  Februari 14, 2026, jijini Dar es Salaam katika  warsha ya kuwajengea uwezo wabunifu na kuwatambua wanufaika wa Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu iliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH)

…………….

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Amier, amewataka vijana wenye ubunifu unaoweza kugeuzwa kuwa bidhaa au huduma kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu, unaosimamiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).

Akizungumza jijini Dar es Salaam Februari 14, 2026, katika warsha ya kuwajengea uwezo wabunifu na kuwatambua wanufaika wa Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu iliyoandaliwa na COSTECH, Naibu Waziri amesema amefarijika kuona tume hiyo imeanza kufanyia kazi changamoto zilizokuwa zinawakabili waombaji, ikiwemo kuanza kuwaandalia mafunzo maalumu kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu mfuko huo na kubaini maeneo yenye ombwe linalosababisha vijana wengi kushindwa kufikiwa na fursa hizo.

“Vijana fanyeni maombi ya kupata fedha hizi, msiogope kujaza fomu hata kama maswali ni mengi. Maswali hayo ni kipimo cha kuonesha kama una nia ya kweli. Unapopatiwa hadi shilingi milioni mia mbili, hicho ni kipimo tosha kwamba una dhamira ya dhati. Fedha zipo,” amesema.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, katika awamu ya kwanza, ilitenga shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wabunifu kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu uliozinduliwa Novemba 2024.

Fedha hizo ni mwendelezo wa hatua za makusudi za kutambua na kuendeleza dhana ya ubunifu nchini.

Mpaka sasa, wizara imetambua wabunifu 3,300 kote nchini kupitia mashindano ya MAKISATU. Kati yao, wabunifu 300 wameendelezwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Ubunifu unaosimamiwa na COSTECH.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema tangu kuzinduliwa kwa mfuko huo, tume imekuwa ikishirikiana na CRDB Foundation katika mchakato wa kuchuja waombaji na kutambua wanaokidhi vigezo.

Waombaji hupimwa kwa pamoja, kisha wanaopitishwa hupatiwa mikopo kwa kuwa Serikali imeweka fedha na pia CRDB Foundation imechangia shilingi bilioni 2.

Amesema wameanzisha mfumo wa mafunzo baada ya kubaini kuwa waombaji wengi hawakuwa na uelewa wa kutosha. Awali kulikuwa na maombi 700 wakati mfuko ulikuwa ukitoa ruzuku, lakini ulipobadilishwa kuwa wa mikopo idadi ya waombaji ilipungua.

Kati ya maombi 63 yaliyowasilishwa, maombi 41 hayakukamilika, waombaji 20 waliona masharti kuwa magumu kutokana na wingi wa maswali, waombaji 8 hawakukidhi vigezo, na wengine hawakuwa na uelewa wa kutosha, taarifa sahihi, ushahidi wa biashara zao wala mazingira rafiki ya uzalishaji.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema wabunifu saba tayari wamekidhi vigezo na wako tayari kukabidhiwa fedha zao kupitia CRDB. Pia amewahimiza vijana kuendelea kutuma maombi ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

“Jana tulikuwa Dodoma ambapo vijana 370 waliwasilisha maombi. Hadi sasa ninapozungumza, vijana 500 wameleta maombi yao. Ninawaomba waendelee kutembelea mitandao yetu ya CRDB Foundation ili kupata taarifa na fursa hizi,” amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post