Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno, amefunga rasmi mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali kuhusu usimamizi na uendeshaji wa miradi ya Uwekezaji na Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public-Private Partnership – PPP).
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wakufunzi kutoka kampuni ya Cybiant kutoka nchini Malaysia yamefungwa rasmi tarehe 6 Februari, 2026 Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga katika kuwaongezea uwezo mawakili hao kuhusiana na mbinu za kisasa za majadiliano (negotiations), uchambuzi wa mikataba, ununuzi na utiaji saini wa mikataba, usimamizi wa mikataba na namna bora ya kupata taarifa za miradi mikubwa ya maendeleo.
*“Mafunzo haya ni nyenzo muhimu kwa Mawakili wa Serikali kuhakikisha kuwa Miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inakuwa na tija na inayolinda rasilimali za nchi.”* Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mhe. Maneno ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Mawakili wa Serikali ili kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali inayoingiwa kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inaendana na utekelezaji wa Dira 2050.
*“kupitia mafunzo haya tunaamini kuwa tutapata Mawakili wenye weledi na ubora mkubwa katika kutengeneza mikataba ya miradi mikubwa itakayosaidia kutengeneza mazingira rafiki ya uwezekezaji kuelekea utekelezaji wa Dira 2050”*.Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Bw. Ildephonce Mukandara kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo ameushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuongeza ujuzi katika Upekuzi wa Mikataba ya Ubia na kuisaidia Serikali katika utekelezaji wa Dira 2050.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mikakati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kuwa Watumishi wake wanaongeza ujuzi utakaowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

