NAIBU KATIBU MKUU MAZINGIRA ARIPOTI OFISI YA MAKAMU WA RAIS

 

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Baraka Luvanda amepokelewa rasmi katika Ofisi za Makamu wa Rais baada ya kuapishwa Ikulu, jijini Dar es Salaam leo Februari 09, 2026.  

Hafla hiyo ya mapokezi imefanyika katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais Luthuli jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muuungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange.

Akizungumza awali akimpokea Balozi Luvanda aliyefika ofisini kwake kujitambulisha, Mhe. Dkt. Dugange amekaribisha Balozi Luvanda na kumtakia kila la heri katika majukumu yake ya kusimamia Mazingira kwenye Ofisi hiyo.

Amesema yapo mengi katika sekta hiyo muhimu ya mazingira ambayo kwa nafasi yake atakuwa na jukumu la kuyasimamia kuhakikisha mazingira yanakuwa endelevu.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi alimuahidi Balozi Luvanda ushirikiano mkubwa ambao utamuwezesha kufanya shughuli zake kwa ufanisi.

Aliwaomba watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kumpa ushirikiano Balozi Luvanda katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema Ofisi itaendelea kuimarisha Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) ili kuhakikisha Serikali inafaidika na biashara ya kaboni kwa kuleta fursa.

Kwa upande wake Balozi Luvanda akizungumza na sehemu ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata.

Alionesha dhamira yake ya kufanya kazi kwa karibu na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, hususan katika masuala ya Muungano na Usimamizi wa Mazingira.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo utaongozwa na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia Sera, Sheria na Mikakati ya Taifa inayolenga maendeleo endelevu.  

Post a Comment

Previous Post Next Post