TANZANIA KUNUFAIKA NA UMAKANU WA RAIS WA BARAZA LA MAZINGIRA DUNIANI (UNEA)

 

Kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA) kutaiwezesha nchi kunufaika na fedha kutoka Mifuko mbalimbali ya Mazingira duniani.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati akijibu maswali bungeni pamoja na kutoa shukrani kwa wabungeni kwa pongezi za kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa UNEA.

Alisema hatua hiyo ni heshima kubwa kwa Tanzania katika Jumuiya ya Kimataifa ambayo imechagizwa na kazi kubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa anayofanya katika sekta ya mazingira.

Mhandisi Masauni alifafanua kuwa Tanzania itaweza kupenyeza vipaumbele vyake vya mazingira katika mikutano mbalimbali ya kimataifa kwa kutafuta fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

“Mheshimiwa Spika kwa nafasi hii tuliyopata kama Taifa tutaweza kupata fedha za kukabiliana na upotevu wa bioanuwai, za kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na fedha za Mifuko mbalimbali kutoka Jumuiya ya Kimataifa,” alisema.

Mhandisi Masauni alichaguliwa kushika nafasi hiyo wakati wa Mkutano wa saba wa Baraza hilo uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), jijini Nairobi, Kenya Desemba 12, 2025.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Masauni aliliriafu Bunge kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini katika Maziwa Babati, Basotu na Tlawi mkoani Manyara kupata suluhisho la kuwepo kwa magugu maji.

Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Zacharia Isaay aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatembelea na kukagua maeneo ya maziwa yaliyoathiriwa na magugu maji mkoani Manyara.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Masauni alisema pamoja na hatua hiyo pia Serikali inatarajia kununua mitambo ya kukabiliana na tatizo la kukithiri kwa viumbe vamizi hivyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post