Kilimo Bora Chachochea Tija na Uzalishaji kwa Wakulima

Mwandishi Wetu,

Wakulima wa Kijiji cha Matui  kilichopo Halmshauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manayara wamehimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo hususan mbolea, ili kuongeza tija na kuboresha maisha yao kupitia kilimo chenye tija na cha kibiashara.

Wito huo umetolewa tarehe 23 Februari , 2026 wakati wa kampeni ya Mali Shambani inayofanywa  na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi zake,  yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya pembejeo na kuongeza uelewa kwa wakulima kuhusu kanuni bora za kilimo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Udhibiti Ubora kutoka TFRA, Said Athuman, alisema lengo kuu la kampeni hiyo ni kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo  pamoja na kuhamasisha wakulima kuzitumia  kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo. Alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mbolea huanza na upimaji wa afya ya udongo ili kubaini mahitaji halisi ya virutubisho kabla ya matumizi.

Aidha, alisema TFRA inaendelea kuhamasisha wakulima kujisajili katika mpango wa ruzuku ya mbolea na kushirikiana kwa karibu na maafisa ugani wa vijiji na kata ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu umuhimu wa mbolea katika kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake mkulima wa kijiji hicho, Zubeda Bakari Kalanga, alisema mafunzo hayo yamebadili mtazamo wake kuhusu matumizi ya mbolea, akieleza kuwa awali aliamini mbolea za viwandani huharibu udongo, lakini sasa ameelewa kuwa matumizi yasiyo sahihi ndiyo husababisha madhara. 

Aliongeza kuwa tofauti ya mavuno ni kubwa kati ya mkulima anayetumia pembejeo sahihi na asiyetumia, akibainisha kuwa licha ya kulima eneo dogo, mavuno yake yameongezeka kutokana na matumizi sahihi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu.

Uhamasishaji huo unaendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika uzalishaji na maendeleo ya sekta ya kilimo.


Post a Comment

Previous Post Next Post