DAWASA YASISITIZWA KUTAFUTA VYANZO MBADALA VYA FEDHA

Mwandishi Wetu,

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesisitiza haja ya kuongeza msukumo katika upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maji ili kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya uhakika, yenye ubora na endelevu.

Akizungumza katika kikao kazi cha viongozi waandamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), jijini Dar es Salaam, Waziri Aweso amesema Serikali itaendelea kuharakisha michakato ya upatikanaji wa mikopo nafuu kutoka kwa wahisani, pamoja na kuwezesha mbinu mbadala za ufadhili wa miradi (Alternative Project Financing) kwa miradi mikubwa yenye manufaa mapana kwa sekta mbalimbali.

Ameitaja baadhi ya miradi ya kimkakati inayopewa kipaumbele kuwa ni ukamilishaji wa Mradi wa Bwawa la Kidunda, upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini na Mradi wa Kutoa Maji Kutoka Mto Rufiji, ameeleza kuwa miradi hiyo ni muhimu katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa maji, hasa wakati wa kiangazi.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunapata rasilimali za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii, sanjari na kuboresha huduma kwa wananchi,” Aweso amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutekeleza mkakati wa kupunguza na kudhibiti upotevu wa maji, ikiwemo kukomesha wizi wa maji, pamoja na kujenga uwezo wa watumishi na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kazi ili kuwaongezea ufanisi katika majukumu yao.

Pia, ameitaka DAWASA kupitia upya Mkakati wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma ili wananchi wawe na uelewa mpana wa hali ya huduma na hatua zinazochukuliwa na Serikali.

Waziri Aweso amehitimisha kwa kutoa rai kwa wadau na wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa uharibifu wa rasilimali za maji haupaswi kuvumiliwa na sheria zilizopo lazima zisimamiwe ipasavyo ili kulinda rasilimali hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesistiza umuhimu wa kuongeza ufanisi kwa watendaji wa DAWASA na kuimarisha mifumo ya usimamizi na uwajibikaji ili kukidhi matarajio ya wananchi na kuchochea maendeleo ya Sekta ya Maji.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Rose Ambrose, amewataka viongozi wa Sekta ya Maji kuweka mipango thabiti itakayotoa matokeo chanya kwa wananchi na kutatua changamoto za huduma ya maji nchini.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuweka mipango na mikakati madhubuti ya usimamizi na utoaji huduma endelevu za maji kwa wananchi katika Mikoa ya Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Pwani.


Post a Comment

Previous Post Next Post