CUF- Chama Cha Wananchi kimepokea taarifa zinazosambazwa na wasiokitakia mema Chama juu ya uwepo wa Mkutano Mkuu wa dharura unaoambatana na wito kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwenda kwa Msajili wa Vyama kesho jumatatu Februari 9, 2026 au katika siku nyingine yoyote inayotajwa. Tunatumia fursa hii kuwataarifu wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Taifa, wanachama, waandishi wa habari na watanzania wote kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote na zipuuzwe.
Kwa mujibu wa Ibara za 72(2) na 72(3) za Katiba ya CUF- Chama Cha Wananchi ya 1992 Toleo la 2019 na marekebisho yake ya 2024, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) ndicho Chombo chenye Mamlaka ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Taifa wa dharura, hata pale ambapo mkutano huo utaitishwa kwa makubaliano ya zaidi ya nusu ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kutoka kila upande wa Muungano
na, kwa vyovyote vile Msajili wa Vyama vya Siasa anapaswa kuutambua na kualikwa rasmi, kama ilivyo kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa.
BKUT katika Kikao chake cha Desemba 17 na 18 hakijaazimia kuitisha Mkutano Mkuu wa dharura na pia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekana kupokea taarifa yoyote ya mkutano huo haramu, wala kuwaita wanachama wa CUF- Chama Cha Wananchi Ofisi ya Msajili.
Utafiti ambao Chama kimeufanya umebaini kwamba wanaopigia wajumbe simu za mialiko ni vibaraka wa baadhi ya watu wasio waaminifu wanaoumizwa na Msimamo Madhubuti wa CUF- Chama Cha Wananchi ulioanza kuwekwa bayana na Mwenyekiti Taifa Prof. Ibrahim Lipumba Novemba 5, 2025 na kuendelezwa na BKUT kwenye Kikao cha Desemba 17 na 18, 2025 . Msimamo wa CUF -Chama Cha Wananchi kutaka iundwe Serikali ya Mpito ya Kulea Taifa kama njia pekee ya kutegemewa ya kulirudisha Taifa pamoja baada ya Uchaguzi Mkuu bandia na Mauaji ya Oktoba 29, 2025 ni Msimamo wa dhati kuhusu Maridhiano ya Kweli, kama ulivyofafanuliwa kwenye RASIMU ya Serikali ya Mpito inayopendekezwa na Chama kupitia Wasilisho kwenye Kongamano la Kumbukizi ya Mauaji ya Januari 26 na 27, 2001 lililofanyika Buguruni Januari 27 mwaka huu.
Wasiokitakia mema Chama wanadhani wanaweza kuyazima mapambano haya ya kudai Demokrasia ya Kweli na Utawala wa Sheria kwa kuanzisha migogoro ndani ya Chama, hususan dhidi ya Jemedari Prof. Ibrahim Lipumba.
Mkutano wowote unaoitishwa nje ya utaratibu ni chanzo cha vurugu na uvunjifu wa Amani. Tunatoa wito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi nchini, kuchukua hatua stahiki kuhakikisha hakuna mikusanyiko ya aina hiyo na kwa vyovyote vile watabeba lawama kwa chochote kile kitakacholazimika kufanywa na wanachama wa CUF-Chama Cha Wananchi kudhibiti mikusanyiko hiyo isipodhibitiwa na vyombo husika.
Tunawakumbusha wanachama wetu waendelee kufanya Tafakuri ya Kina juu ya RASIMU ya Serikali ya Mpito katika maeneo yao ili waweze kutoa michango yao wakati wa Mjadala wa Kitaifa ambao kama Chama tunaupigania kwa maslahi ya Tanzania. Aidha tunawakumbusha wote wenye kujaribu kuratibu Mapinduzi ndani ya Chama kwa kutumia nguvu yoyote ile kwamba Tanzania imeshajeruhiwa na kila patakapotumika matumizi ya nguvu haramu kwa maslahi ya yeyote, tutakuwa tunaongeza ukubwa wa majeraha.
HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!
Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Februari 8, 2026```
.jpeg)