
Mwandishi Wetu Cape Town Afrika Kusini,
Sekta ya Madini Tanzania imeendelea kudhihirisha mwelekeo chanya wa ukuaji na uimarikaji wa kimkakati kufuatia mwendelezo wa vikao vya Wizara ya Madini na wadau wa kimataifa katika Kongamano la Mining Indaba 2026 linaloendelea jijini Cape Town, nchini Afrika Kusini.

Majadiliano mbalimbali yaliyofanyika Februari 11, 2027 yameakisi dhamira thabiti ya Serikali ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, kukuza ushiriki wa wazawa, wanawake na vijana, pamoja na kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia kwa tija katika uchumi wa Taifa na maendeleo endelevu.
*EU Kushirikiana na Tanzania kwenye Mnyororo wa Thamani wa Madini*
Umoja wa Ulaya (EU) umeonesha nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, ikiwemo ujenzi wa uwezo kwa wataalam wa madini, mafunzo ya ufundi stadi, teknolojia za kisasa, na utunzaji wa data na takwimu. EU imebainisha kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na programu ya PanAfGeo inayotekelezwa kupitia EuroGeoSurveys. Programu hiyo ni mpango wa Umoja wa Ulaya (EU) unaolenga kuimarisha uwezo wa Taasisi za Utafiti wa Jiolojia barani Afrika, ikiwemo Tanzania, ili kusaidia maendeleo endelevu ya sekta ya madini.
Aidha, Umoja huo umeahidi kushirikiana na Serikali katika kutafuta masoko ya madini barani Ulaya na kuwatengenezea mazingira wezeshi wawekezaji ili waweze kutekeleza shughuli za uongezaji thamani madini ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa haraka wa miradi ya madini na kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
*Mavunde Asisitiza Utayari wa Tanzania na Afrika Kushirikiana na wawekezaji, Sekta Binafsi*
Akitoa hotuba yake maalum ya ufunguzi wa siku ya pili ya kongamano la Mining Indaba 2026, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Tanzania na Afrika kwa ujumla ziko tayari kushirikiana na wawekezaji na sekta binafsi katika kuvuna rasilimali za madini kwa manufaa ya pamoja. Ameeleza kuwa Afrika inalenga kubadilika kutoka kusafirisha madini ghafi kwenda katika uongezaji thamani ndani ya nchi zake.
Akijenga hoja yake, Waziri Mavunde amesema kuwa mjadala wa resource nationalism kuhusu bara la Afrika mara nyingi hutafsiriwa isivyo, akifafanua kuwa mtazamo wa Afrika kuhusu usimamizi wa rasilimali haulengi kuwatenga wawekezaji, kuleta kutokutabirika kwa sera au kutafuta faida za muda mfupi, bali unasimamia rasilimali kwa uwajibikaji, uwazi na kwa kuzingatia sheria, ili ziwe chachu ya maendeleo ya muda mrefu kwa nchi husika na wananchi wake.
Akitoa mfano wa Tanzania, Mhe. Mavunde alisema msimamo huo si kikwazo cha uwekezaji bali ni msingi wa kujenga ushirikiano endelevu. Alisisitiza kuwa usimamizi wa kweli wa rasilimali unahusisha kuheshimu mikataba na mifumo ya kisheria, kutoa uhakika na utabirikaji wa sera kwa wawekezaji, kuhakikisha thamani ya haki kwa mataifa ya Afrika na jamii zinazozunguka miradi ya madini, pamoja na kuhimiza uongezaji thamani na uwekezaji wa muda mrefu katika mazingira yenye taasisi imara, sera thabiti na uhalali wa kijamii.
Mhe. Anthony Mavunde alisisitiza kuwa Dira ya Madini ya Afrika, ajenda ya maendeleo ya Tanzania (Tanzania Development Vision), na kaulimbiu ya Indaba zote zinakutana kwenye msingi mmoja wa kwamba “ushirikiano ni daraja kati ya dira na mitaji”. Alibainisha kuwa madini yanahitaji mitaji, ushirikiano baina ya serikali na wawekezaji, na mipango ya miundombinu, huku akisisitiza kuwa Tanzania inajenga ushirikiano katika msingi wa kuaminiana, uwazi na mgawanyo sawia wa manufaa kwa kila upande.
*Baririck Yatoa Msukumo Mpya Sekta ya Madini*
Katika kikao kilichofanyika baina ya Waziri wa Madini na kampuni ya Barrick Mining Corporation, kampuni hiyo imeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuhaulisha ujuzi kwa wafanyakazi wa wizara kupitia mafunzo ya vitendo katika fani na ujuzi mbalimbali unaohitajika kwenye sekta ya madini.
Kupitia kikao hicho, Mhe. Waziri ameishukuru Barrick Mining Corporation kwa kudumisha desturi ya ushirikiano wake na Serikali na kusisitiza matarajio ya Serikali kuona manufaa makubwa zaidi kwa Taifa kutokana na uwepo wa kampuni hiyo nchini.
Waziri Mavunde pia ameelezea programu ya Mining For A Brighter Tomorrow inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu na kwa tija katika uchumi wa madini na kupongeza ushiriki wa Barrick kwenye programu ya vijana wa Nyamongo.
*Kampuni ya SOTTA kuzalisha dhahabu ya kwanza 2027*
Ujumbe wa Kampuni ya Sotta Mining Corporation, inayomiliki mradi mkubwa wa uchimbaji wa dhahabu wa Nyanzaga wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, umeishukuru Serikali kwa ushirikiano unaotolewa katika kuendeleza mradi huo. Kampuni hiyo imeomba majadiliano zaidi ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa wazabuni wazawa kwa ajili ya kutoa huduma kwenye mgodi huo.
Akijibu ombi hilo, Mhe. Mavunde ameahidi Serikali kukaa pamoja na wawekezaji hao kutafuta suluhisho la changamoto hizo kwa kuzingatia misingi ya sheria. Aidha, ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha mradi unatekelezwa ndani ya muda uliopangwa, huku uzalishaji ukitarajiwa kuanza katika robo ya kwanza ya mwaka 2027.