REA KUZINDUA KITUO CHA KUPOZA NA KUSAMBAZA UMEME CHA MTERA, KUHUDUMIA WILAYA 3

 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Eng. Hassan Saidy, akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya REA Jijini Dodoma, Januari 15, 2026, kuelekea uzinduzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Mtera pamoja na tukio la kusaini mikataba ya kupeleka umeme vitongojini.

Na. Meleka Kulwa 

‎Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi  Hassan Saidy, amesema kuwa uzinduzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Mtera ni mradi wa kimkakati unaolenga kuboresha upatikanaji wa umeme katika wilaya za Kongwa, Mpwapwa na Iringa. 

‎Amesema kuwa uzinduzi rasmi wa kituo hiki utafanyika Januari 16, Jijini Dodoma, na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati,Mhe. Deo Ndejembi, ikiwa ni hatua nyingine muhimu katika mpango wa Taifa wa Nishati ya Umeme vijijini.

‎Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu Wa REA,Eng. Hassan Saidy alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Makao Makuu ya REA Jijini  Dodoma, Januari 15, 2026 

‎Pia, Eng. Saidy amesema kuwa kituo hiki kilijengwa kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 9.7 kwa msaada wa Serikali ya Tanzania pamoja na mchango wa Serikali za Sweden na Norway. Amesema kuwa mradi huu umepunguza tatizo la low voltage, kupunguza kwa kiasi kikubwa kukatika kwa umeme, na kuimarisha usambazaji kutoka Mtera hadi Dodoma na Iringa.

‎Aidha, Mkurugenzi Mkuu, Eng.Saidy amesema kuwa ujenzi wa kituo umejumuisha transfoma mbili za MV kumi kila moja, chumba cha “Swaggz Room” kwa ajili ya njia za umeme, mfumo wa “Break Control” na “Communication System.” Amesema kuwa kituo hiki kinatoa fursa kwa TANESCO kutoa huduma bora, kuongeza uwezo wa usambazaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo viwanda vikubwa na huduma kwa wananchi wa vijijini.

‎Eng. Saidy amebainisha kuwa mradi mwingine mkubwa ni kupeleka umeme kwenye vitongoji, unaohusisha vitongoji Zaidi ya 9000 kote nchini. Amesema kuwa tangu mwaka 2021, vitongoji 28,000 vimepatiwa umeme, huku vitongoji 13,445 vikiwa kwenye miradi inayoendelea. Aidha amebainisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 1.2 na utatoa ajira zisizopungua 4,600 moja kwa moja kwa wananchi wa vijijini.

‎Aidha amebainisha kuwa ujenzi wa vituo vidogo vya kupoza umeme  katika maeneo kama  Mtwara, Hanang, Nzega na Mbarali mchakato wa kujenga vituo maeneo hayo unaendelea na pindi utakapo kamilika Ujenzi utaanza, huku dhamira ya REA ikiwa ni kuhakikisha kila wilaya nchini Tanzania ina kituo kidogo cha kupoza umeme. 

‎Aidha amebainisha kuwa miradi hii itasaidia kuunganisha shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na pampu za maji, hivyo kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesema kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa hii katika kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.

‎Eng. Saidy ameongeza kuwa matukio haya yanaonyesha jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kila mwananchi wa Tanzania anapata huduma ya umeme bila kujali eneo analoishi.

‎Kwa upande mwingine, Eng. Saidy, amebainisha kuwa REA pia inatarajia kusaini mikataba ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji takribani 9,000 kote nchini, tukio litakalofanyika Jumamosi 17,2026  katika Ukumbi wa Hazina Ndogo, Jijini Dodoma. 

‎Mkurugenzi Mkuu wa REA, Eng. Saidy, amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kupitia mikataba 30 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, kwa gharama ya takribani shilingi trilioni 1.2, na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu, ukilenga kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini.   

Post a Comment

Previous Post Next Post