ETDCO YASAINI MIRADI YA REA KUUNGANISHA UMEME VITONGOJI 620

Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) Mustapha Himba (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy wakionesha mikataba baada ya kusaini utekeleza wa miradi ya Kusambaza Umeme katika Vitongoji 620 vya Mikoa ya Katavi na Ruvuma, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 95.2 iliyofanyika Januari 17, 2026 jijini Dodoma.

Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) Mustapha Himba na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy wakipongezana baada ya kusaini mikataba wa utekeleza wa miradi.
Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja akiwa katika hafla ya utiaji saini wa mikataba kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini.
Waziri wa Nishati, Mhe.  Deogratius Ndejembi (katikati)akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali katika hafla ya utiaji saini wa mikataba kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini.
………….
Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umeme (ETDCO) imesaini mikataba ya kutekeleza miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ya Kusambaza Umeme katika Vitongoji 620 vya Mikoa ya Katavi na Ruvuma, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 95.2.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika Januari 17, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Mhe.  Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa uadilifu na usimamizi thabiti ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Mhe. Ndejembi amesema utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amewataka wakandarasi kuzingatia ubora wa kazi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwapatia Watanzania huduma ya umeme ya uhakika.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, ameishukuru Wizara ya Nishati pamoja na REA kwa imani waliyoipa Kampuni hiyo, huku  akieleza kuwa ETDCO imejipanga kutekeleza miradi kwa wakati na  kuzingatia masharti ya mikataba.
Amesema miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu  ambapo  itanufaisha wananchi  wa awali takribani 19,950 katika Mikoa ya Katavi na Ruvuma.
Amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 500 ikiwemo za  moja kwa moja, huku wananchi wa maeneo husika wakihimizwa kuchangamkia fursa hizo.
Kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa za kijamii na kiuchumi, kuimarisha shughuli za maendeleo, na kuchangia ustawi endelevu wa Taifa

Post a Comment

Previous Post Next Post